Dar es Salaam. Mchakato wa kura za maoni za udiwani wa viti maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliohitimishwa Julai 20, mwaka huu, umeongeza joto la kuwapata wagombea watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwenye nafasi ya udiwani, uwakilishi na ubunge.
Joto linaongezeka kwa sababu katika kura za maoni za kuwapata madiwani wa viti maalumu, wapo wanaoungwa mkono na watiania wa ubunge, uwakilishi na udiwani wa kata.
Kutokana na mazingira hayo, ikitokea unayemuunga mkono katika ngazi ya udiwani viti maalumu ameanguka, inatoa wakati mgumu kwa mtiania wa ubunge au uwakilishi.
Mbali na hilo, joto hilo linachochewa zaidi baada ya madiwani wa viti maalumu wakongwe na wanaotetea nafasi zao kudaiwa kuangushwa katika mchakato wa kura za maoni uliofanyika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.
Hali hiyo inatajwa kuwapa wakati mgumu baadhi ya watiania wa udiwani, uwakilishi na ubunge waliokuwa wakiwaunga mkono wagombea hao, jambo linalodaiwa kusababisha wagombea hao kubadili mbinu katika vita ya kupata uungwaji mkono pindi majina yao yatakaporejeshwa na Kamati Kuu.
Kwa sasa, wagombea wa udiwani, uwakilishi na ubunge wanasubiri uteuzi wa majina matatu, kazi itakayofanywa na Kamati Kuu ya CCM itakayoketi Julai 28 ili kufikiria na kuteua majina ya watiania wasiozidi watatu wakapigiwe kura za maoni.
Taarifa ambazo Mwananchi limezipata kutoka maeneo mbalimbali zinadai baadhi ya maeneo, hususan Kanda ya Kati, matokeo ya udiwani huo wa viti maalumu yalipinduliwa kutokana na kasoro zilizosababishwa na vitendo vya rushwa.
Hii inaelezwa kuwa inaweza kuangaliwa kwa kina kwenye michakato ya vikao kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa, ambako utafanyika uteuzi wa mwisho.
Awali, mchakato wa uteuzi wa majina matatu ya watiania wa udiwani, uwakilishi na ubunge ulitakiwa kufanyika Julai 19, lakini ulisogezwa mbele kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo idadi ya wagombea kama ilivyoelezwa na Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla.
Hata hivyo, mabadiliko hayo ya ratiba yanatajwa kuongeza mrundikano wa shughuli za chama hicho ndani ya siku chache, hivyo kuweka nafasi ndogo ya watiania na viongozi wa CCM kupumua.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kufikiria na kuteua majina ya watiania wasiozidi watatu kwa ubunge, uwakilishi na udiwani ili wakapigiwe kura za maoni, kitafanyika Julai 28.
Kikao hicho kitatanguliwa na Kamati ya Usalama na Maadili Taifa, Julai 27. Kisha, Julai 30, mikutano mikuu maalumu ya mikoa ya UWT kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa viti maalumu Bara na Zanzibar vitafuata ngazi ya mikoa.
Agosti mosi, utafanyika Mkutano Mkuu Maalum wa UVCCM Taifa asubuhi kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge/uwakilishi Bara na Zanzibar na jioni Mkutano Mkuu Maalumu wa Wazazi Taifa, kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge/uwakilishi Zanzibar na Bara.
Mkutano huo utafuatiwa na Mkutano Mkuu Maalum wa UWT Taifa kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge wa viti maalumu vya makundi (Tanzania Bara) na ubunge/uwakilishi viti maalumu (Zanzibar), Agosti 2, 2025.
Kinachoendelea kwa sasa majimboni na kwenye kata ni kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kwa kila mtiania, baada ya mabadiliko ya ratiba na hofu ya kuanguka.
Kwa sasa ni kawaida kuwaona wabunge wanaotetea nafasi, wakiwemo mawaziri wa wizara nyeti, wakipiga picha na kuziposti katika mitandao ya kijamii zikiwaonyesha wapo karibu na wapigakura.
Wanafanya hivyo ikiwa ni mbinu ya kujihakikishia hatima njema kuelekea michakato ya ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, si maeneo yote watiania wamepiga kambi, bali kuna sehemu zilizokuwa na wagombea wengi, baadhi wameondoka na kurejea katika shughuli zao za kawaida kutokana na kukosa matumaini ya majina yao kurudi kwa wajumbe.
Mmoja wa watiania wa ubunge (jina limehifadhiwa) anasema matokeo ya udiwani wa viti maalumu yamewavuruga baadhi ya wagombea baada ya waliowaunga mkono kushindwa kufurukuta.
“Hawa madiwani ni watu muhimu, ndiyo wanakupa picha halisi ya ushindi wako katika mchakato wa kura za maoni endapo jina lako litarudishwa. Sasa unayemuunga mkono akishindwa, inakupa tafsiri kuwa hali yako si nzuri mbele ya safari.
“Uzuri wa madiwani hao wapo karibu na wananchi na wapigakura (wajumbe), sasa mgombea huwezi kuwafikia wote, lazima uwatumie kupata uungwaji mkono. Ukiwapata madiwani wa kutosha, unakuwa na mtaji mzuri mbele ya safari,” amesema mtiania huyo.
Mmoja wa wajumbe ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini amesema kinachoendelea kwenye uwanja wa siasa ni kuwa walioshinda kura za maoni za udiwani wa viti maalumu na kuungwa mkono na baadhi ya watiania wanazidi kuimarisha ngome zao.
“Matokeo ya udiwani huwa yanatoa taswira ya moja kwa moja hadi matokeo ya ubunge na uwakilishi, hivyo ukaribu unazidi kuendelea baina yao na watiania ili kuimarisha ushirikiano,” amesema.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, madiwani wanawajua wapigakura kutoka katika maeneo yao, hasa katika kipindi hiki ambacho vyombo vya chama vinadaiwa kuwa vipo kazini kuchunguza walioongoza kura za maoni kama wametumia rushwa au la.
“Hivi sasa walioshindwa kura za maoni za udiwani wa viti maalumu wanachunguzwa, lakini wagombea wa ubunge na udiwani wametengeneza ngome na wanawasiliana namna ya kujikusanyia kura pindi mchakato utakapoanza,” amesema.
Amesema watiania wa ubunge na uwakilishi wakitengeneza uhusiano na madiwani wa viti maalumu, mara nyingi huwa hawazunguki ovyo mitaani kuogopa kuharibiwa sifa.
“Mikakati hiyo inafanyika kwa siri, ni vigumu kujua kwa sababu ni mipango iliyosukwa kwa muda mrefu. Sasa hivi watiania wa ubunge na uwakilishi kazi wanayofanya ni kuimarisha ngome zao kama mtu wao ameshinda, ingawa walioanguka hali yao ni mbaya,” amesema.