Jeshi la Polisi mkoa wa Lindi linamshikilia mwanaume aitwaye Araba Samali Chichonyo (57), mkazi wa Kijiji cha Juhudi “A”, Kata ya Chinongwe, Wilaya ya Ruangwa kwa tuhuma za kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 78, ambaye pia ni mkazi wa kijiji hicho. Tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kutokea usiku wa Julai 20, 2025, majira ya saa nne, nyumbani kwa muhanga, wakati walipokuwa wakinywa pombe ya kienyeji aina ya wanzuki.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, mtuhumiwa alikuwa ameajiriwa na muhanga huyo kuchimba shimo la choo kwa makubaliano ya ujira wa shilingi elfu kumi. Awali, muhanga alimlipa mtuhumiwa shilingi elfu saba, na siku ya tukio alikabidhiwa shilingi elfu mbili kati ya elfu tatu zilizokuwa zimebaki. Baada ya kulipwa kiasi hicho, mtuhumiwa alikwenda kununua pombe hiyo ya kienyeji na kurejea nyumbani kwa muhanga, ambapo waliendelea kunywa pamoja na mume wa muhanga ambaye ni mlemavu wa macho.
Ilielezwa kuwa wakati wakiendelea na unywaji wa pombe, na mume wa muhanga akiwa amelewa na kupoteza fahamu, mtuhumiwa alitumia mwanya huo kumvamia muhanga. Alimshika kwa nguvu, kisha kumvua nguo ya ndani na kutekeleza kitendo hicho cha ukatili wa kingono ukumbini hapo walipokuwa wamekaa. Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alitoroka kusikojulikana.
Hata hivyo, kwa juhudi za Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho, walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo, ambaye sasa anashikiliwa na Polisi kwa ajili ya mahojiano na hatua za kisheria kuendelea. Kamanda wa Polisi mkoa wa Lindi amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kufichua vitendo viovu, huku akisisitiza kuwa sheria itachukua mkondo wake bila upendeleo.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa jamii kuheshimu utu wa binadamu, hasa kwa wazee na watu wasiojiweza, na kuonya kuwa vitendo vya ukatili havitavumiliwa kamwe katika jamii inayozingatia misingi ya haki na maadili.