BAADA ya kuitumikia Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Simba, inaelezwa kiungo mkabaji Jonas Mkude anaungana na aliyekuwa kocha wake, Miguel Gamodi.
Mkude ni sehemu ya nyota waliomaliza mkataba Yanga ulipomalizika msimu wa 2024-2025 huku chanzo cha kuaminika kutoka Singida Black Stars kikiliambia Mwanaspoti kiungo huyo atakuwa sehemu ya kikosi chao msimu ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, mtoa taarifa huyo alisema ni kweli Mkude amefikia hatua ya mwisho kusaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo baada ya kumalizana na Yanga huku Gamondi akitajwa kuhusika kumvuta kikosini hapo.
“Kocha Gamondi ndiye aliyependemeza kusajiliwa kwa kiungo huyo licha ya kwamba hakuwa na namba kikosi cha kwanza cha Yanga, amekiri kuwa ni miongoni mwa wachezaji bora ambao amewahi kufanya nao kazi,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.
“Mbali na Mkude, pia Gamondi alisisitiza kusajiliwa kwa Nickson Kibabage ambaye anarejea pia baada ya kuondoka misimu miwili aliyoitumikia Yanga kwa mafanikio akipata nafasi ya kucheza mbele ya kocha huyo.”
Chanzo hicho kiliekeza, ujio wa nyota hao Singida Black Stars ni sehemu ya kujiandaa na kuimarisha kikosi chao tayari kwa ajili ya michuano ya ndani na kimataifa.
“Mkude na Kibabage wote wana uzoefu na kocha alisisitiza kusajiliwa wachezaji ambao tayari wana uzoefu na wana ubora wa kuonyesha ushindani kwenye mashindano ya ndani na nje.”
Kuhusu Kibabage, Mwanaspoti lilisharipoti awali anarudi Singida Black Stars na Yanga inatafuta beki mwingine mzawa kwa ajili ya kusaidiana na Chadrack Boka ambaye tayari imemalizana na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kutoka Simba.
Mkude alitua Yanga 2023-2024 sambamba na Kocha Gamondi na katika kipindi cha misimu miwili aliyocheza, kiungo huyo ametwaa mataji mawili ya Ligi Ku Bara na mawili Kombe la FA, pia Ngao ya Jamii 2024 kama ilivyo kwa Kombe la Muungano, huku akicheza mechi 14 za ligi, kumi msimu wa kwanza na nne msimu uliomalizika hivi karibuni.