Wakati Watanzania wakijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025, mijadala ya kisiasa imetawala majukwaa mbalimbali, hususani kwenye mitandao ya kijamii.
Kauli za kisiasa kama vile No reforms, No election; Oktoba Tunatiki; Piga kura, Linda kura na zingine zimekuwa maarufu mitandaoni.
Kauli hizi na zingine za namna hiyo zinazoibuka kupitia mitandao ya kijamii kama vile X, Facebook na TikTok si maneno ya kupita tu, bali ni alama za msimamo, mwelekeo wa fikra na sauti ya matabaka mbalimbali ya kijamii. Kila moja ina asili, maana na madhumuni mahususi.
No reforms, No election (Bila mabadiliko, Hakuna uchaguzi) inatoa wito wa kufanyika mageuzi ya kisiasa na kisheria hasa katika mifumo ya uchaguzi kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Chini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kauli hiyo inashinikiza mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
Mbali ya Chadema, makundi ya wanaharakati na baadhi ya viongozi wa dini na wasomi wanaotetea haki za kiraia wamekuwa wakisukuma ajenda hiyo.
Oktoba Tunatiki ni kauli inayotumiwa na makada, wapenzi na wakereketwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuonyesha msisitizo wa ushiriki katika Uchaguzi Mkuu, tiki ikiwa alama ya kuidhinisha au kuchagua, hasa wakati wa kupiga kura.
Ni kauli inayosisitiza kuwa, licha ya changamoto, bado wananchi wana wajibu wa kuamua mustakabali wao kupitia sanduku la kura, ikilenga kushawishi ushiriki wa vijana na watu waliovunjika moyo kisiasa.
Inatumiwa na makundi yanayounga mkono mabadiliko kupitia sanduku la kura, wakiwamo wanachama wa vyama vya siasa, mashirika ya kiraia na hata baadhi ya wapigakura.
Kauli ya Piga, Linda kura inashabihiana na ya awali ya Oktoba tunatiki, ikisisitiza si tu kushiriki kupiga kura, bali pia kuhakikisha kura hiyo inalindwa na kuhesabiwa kwa haki, ikihamasisha wananchi kuwa makini na mchakato mzima wa uchaguzi.
Vilevile, kauli hiyo inayotumiwa na ACT-Wazalendo inahimiza uwazi, ufuatiliaji wa kura na kulinda matokeo dhidi ya udanganyifu.
Kauli hizi zimeibuka kama majibu ya kihistoria yakirejea chaguzi zilizopita ambazo baadhi zililalamikiwa na jamii kuhusu haki na uwazi, hivyo wanaozitumia wamejitokeza mapema kutetea misingi ya uchaguzi huru.
Kwa mtazamo wa kijamii, mitandao imewezesha kusambaza ujumbe na kauli za harakati, huku vijana wakiwa mstari wa mbele. Kisiasa, Uchaguzi Mkuu wa 2025 unatarajiwa kuwa na mabadiliko, kauli hizo zikionekana kama silaha ya kimkakati katika kujenga misimamo, maoni na vuguvugu la umma.
Majukwaa ya mitandao ya kijamii yamekuwa chachu ya mijadala ya kina kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa Tanzania, usawa katika uchaguzi, nafasi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na hali ya vyama vya siasa nchini.
Kumekuwa kukiibuliwa mijadala mipya kila uchao, baadhi ikikolezwa na matamko ya wanaharakati, viongozi wa dini, asasi za kiraia au wanasiasa wakongwe nchini.
Hali hii imekuwa na athari katika maisha ya kila siku ya baadhi ya wananchi kwani shughuli nyingine za kijamii na kibiashara zimeanza kupoteza nafasi katika mazungumzo ya umma.
Ni mitazamo ya baadhi ya wananchi kuwa mjadala wa uchaguzi sasa umekuwa kama kampeni ya kitaifa isiyo rasmi, inayojikita zaidi kwenye mitandao ya kijamii badala ya uwanja wa wazi.
Kwa sasa, macho na masikio ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa yako kwenye mwenendo wa maandalizi ya uchaguzi huo, huku matarajio makubwa yakiwa ni kuona uchaguzi huru, wa haki na unaohusisha pande zote kwa usawa.
Wadau kadhaa wa maendeleo na uchumi wanatoa wito kwa jamii kuendeleza mijadala hiyo kwa kuzingatia uwajibikaji na amani, huku wakisisitiza umuhimu wa kutokupuuza shughuli za msingi za kijamii na kiuchumi ambazo ni mhimili wa maisha ya kila siku.
Mhadhiri wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo amesema kauli hizo zimebeba maana mbili kuu; wanaotaka uchaguzi uendelee kama ilivyo na wengine wanadhani uahirishwe hadi mabadiliko yatakapofanyika. Amesema wanaosema Oktoba Tunatiki na Piga kura, Linda kura, wanapendekeza uchaguzi ufanyike kama ulivyopangwa wakati wale wanaosema No reforms, No election wanataka yafanyike marekebisho kwanza kabla ya uchaguzi.
“Wote wanashiriki kitu kimoja, wote wanataka uchaguzi, lakini uchaguzi tuufanyaje, hapo ndipo wanapopishana. Kuna ukaribu kati ya wanaosema No election, No reforms na Piga kura, Linda kura, wote hao wawili hawawezi kuthibitisha namna ya kuzuia uchaguzi au kulinda kura,” amesema.
Mwanazuoni huyo amesema kila atakayejaribu kufanya chochote kati yao, atatafsiriwa kwamba anasababisha uvunjifu wa amani kwani kuzuia uchaguzi lazima kuwe na vurugu za kukwamisha hilo. Pia, sheria za sasa zinaelekeza mpigakura kukaa mita 200 baada ya kupiga kura.
Dk Masabo amesema kauli hizo tatu zinaonyesha kwamba Watanzania wamegawanyika, hawana ajenda ya pamoja kama nchi, kila mmoja anaangalia hoja ya kisiasa ili apate nafasi ya uongozi.
“Changamoto kubwa tuliyonayo hapa nchini ni kwamba, mfumo wetu wa siasa umeelemea katika siasa za vyama na siyo siasa za masuala, mitazamo, hoja na masilahi ya wananchi,” amesema.
Kuhusu kauli hizo kuchukua nafasi kwenye mitandao ya kijamii, Dk Masabo amesema majukwaa ya kisiasa kwa Tanzania yamebanwa, hivyo watu wameamua kuhamia kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu huko angalau wanaweza kusema mambo yao.
Balozi mstaafu wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana amesema kauli hizo zinaakisi ushindani wa kisiasa katika msimu wa uchaguzi, jambo ambalo limekuwa likitokea kila unapofika wakati huo.
“Katika mazingira ya uchaguzi ni kawaida kusikia kauli kinzani, kila chama kinanadi na kutetea wanachosimamia, lakini ni kazi ya wananchi kupima na kuamua wasimame na nani,” amesema Dk Bana ambaye pia alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Amesema Watanzania wa sasa si wale wa enzi za Mwalimu Julius Nyerere kwa sababu wanajua na wanachambua mitazamo hiyo na mwisho wanachagua wa kusimama naye, jambo analosema si vibaya.
“Hili la No reforms, No election, Chadema wamelisema na wamelitetea tumelielewa, japo ni jambo jema, kila mtu anataka mabadiliko lakini wajue kuwa mabadiliko ni mchakato hayatatokea siku moja yote yakakamilika,” amesema.
Amesema: “Waende na mabadiliko taratibu kwa kuangalia mahitaji, uzewekano na utekelezaji wa madai yao. Kwangu mimi ni kawaida kabisa mijadala hii kutawala kwa sasa, maana ni wakati wake.”
Wakili na mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Onesmo Kyauke amesema kauli ya ‘No reforms, No election ni tamko lililochelewa kuzinduliwa na hivyo haliwezi kuwa nyenzo ya kisiasa yenye tija wakati huu ambapo nchi tayari iko kwenye kalenda ya uchaguzi.
Anasema katika mazingira ya sasa, hakuna uwezekano wa kufanya marekebisho makubwa ya Katiba wala sheria zinazohusu uchaguzi, hivyo vyama vya siasa vinapaswa kuwa na mikakati ya muda mfupi inayolenga kushiriki uchaguzi huku vikiendelea kuwasilisha hoja zao kwa mamlaka husika.
Dk Kyauke amefafanua kuwa mabadiliko ya Katiba, sheria na kanuni ni safari ya kisiasa yenye mchakato mrefu, si jambo la shinikizo la haraka kwa njia ya kauli za mitandaoni au majukwaani.
“Ni busara Chadema na vyama vingine kuelewa kuwa kila mabadiliko yanahitaji siasa za kimbinu, uhimilivu wa hoja na ushawishi wa kitaifa. Kwa sasa muda umepita, wanapaswa kujipanga kushiriki na kulinda kura,” amesisitiza Dk Kyauke.
Ameongeza kuwa upinzani wa kweli ni ule unaojitokeza kushiriki mchakato kwa mikakati ya kimkakati, si kupiga darubini ya mabadiliko huku ukitishia kususia. Anaonya kuwa siasa za kususia bila maandalizi ya kitaasisi zinawavunjia matumaini wananchi wanaotegemea upinzani kama chombo cha kuleta mabadiliko.
“Kama kweli wanataka mabadiliko ya kweli, wangekuja na hoja hizi baada ya uchaguzi wa 2020, si sasa ambapo muda umebaki miezi michache,” amesisitiza.
Amesema hauwezi kuzuia uchaguzi maana hiyo namna haipo badala yake unaweza kususa kushiriki uchaguzi.
Kwa upande wake, Dk Paul Loisulie, mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), amesema kauli za ‘No Reforms No Election’, Oktoba Tunatiki na Piga kura, Linda kura yako, zinadhihirisha ishara za mgawanyiko wa kisiasa unaoendelea kujengeka chini kwa chini.
Anasema kauli hiyo inayoenezwa na baadhi ya makundi ya wanasiasa imejikita zaidi katika hisia na si mkakati wa kisiasa wenye muono wa mbali. “Mabadiliko hayapatikani kwa misimamo mikali tu, bali kwa mazungumzo, maridhiano na mashauriano ya kisiasa,” anasema.
Dk Loisulie anasisitiza kuwa iwapo hali hii haitadhibitiwa, Taifa linaweza kuingia kwenye uchaguzi wenye mgogoro wa kiimani na kutokuaminiana baina ya wadau wa kisiasa.
Anasema historia ya Afrika imeshuhudia nchi nyingi zikikumbwa na misukosuko kwa sababu ya chaguzi zisizoaminika, hivyo ni jukumu la mamlaka kuhakikisha kunakuwa na mazingira ya mazungumzo na majadiliano kuhusu madai ya vyama vya siasa.
Anaongeza kuwa si vyema kwa mamlaka kupuuza sauti za upinzani zinazodai mageuzi kwa kutumia kauli ya kuwa muda umepita. Badala yake, serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wanapaswa kuonyesha dhamira ya dhati ya kujenga mazingira yatakayoruhusu uchaguzi wa haki, huru na wa amani.
“Chaguzi ni mihimili ya uhalali wa utawala, na bila kuheshimu madai ya vyama, nchi inaweza kujikuta ikikosa maridhiano ya kitaifa,” anaonya Dk Loisulie.
Kwa maoni ya Dk Loisulie, kauli ya ‘Oktoba tunatiki’ na ‘Piga kura, Linda kura yako’ inapaswa kuchukuliwa kama njia mbadala ya kisiasa inayolenga kulinda ushiriki wa wananchi katika mchakato wa uchaguzi.
Hata hivyo, anashauri kuwa ushiriki huo usiwe wa kura pekee bali ujengwe katika msingi wa kudai mageuzi kwa njia ya kisheria na kistaarabu ili kupunguza sintofahamu kabla ya Oktoba.
Anasema mamlaka zinapaswa kutatua tofauti zilizopo ili kuwapo na uchaguzi huru na wakati, kuepuka mifarakano na uwezekano wa migogoro mikubwa baada ya uchaguzi.
“Tofauti hizi zisipotatuliwa tunaweza kupata madhara kwa sababu hata baada ya uchaguzi kunaweza kuwapo malumbano na kulaumiana baina ya makundi haya,” anasema.