Mzunguko siasa za kushughulikiana umetua kwa Mbowe

Siasa za kutajana majina na kuaibishana (naming and shaming), ndizo zimeshika hatamu Tanzania. Nyakati baada ya nyakati, kunakuwa na mtu anamulikwa kama adui wa ndani, anayetumika kudhoofisha upinzani.

Mtindo wa kutajana majina na kuaibishana, umegeuka tabia ya siasa za nchi. Ujenzi wa mazoea, umefanya mijadala ya masuala yenye kuhusu uelekeo wa nchi, ufumbuzi wa matatizo na mikwamo, isiwe na nguvu mbele ya siasa za kushughulikiana.

Mathalan, deni la taifa limefikia Sh107.7 trilioni. Mjadala unapaswa kuwa ni kwa nini deni linaongezeka? Mikopo ina faida au hasara? Kuna namna yoyote ya kufanya ili kuendesha Serikali kwa ufanisi bila mikopo? Upi uwezo wa nchi kumudu madeni? Je, madeni yanasogeza hatari au nuru? Ongeza hoja nyingine kama hizo.

Badala yake, shutuma zinaelekezwa moja kwa moja kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Mjadala hauwi kuhusu mikopo na faida au hasara zake. Anashughulikiwa anayeongoza Serikali inayokopa. Ni siasa mbaya, zinachafua, zinasimanga na zinadhalilisha, kuliko kusaidia nchi.

Kwa mtindo huo wa siasa, muda utafika, Rais Samia, hatakuwa Ikulu. Jambo ambalo linatabirika haraka ni kwamba wakati huo, mashambulizi yatamwelekea kiongozi aliye madarakani. Ni kwa sababu ya ulemavu wa kisiasa ambao umetengenezwa na unaendelea kushika kasi.

Lawama kutoka rais hadi rais, kwenye siasa za upinzani nako ni patashika. Zimepita nyakati ambazo jina la Zitto Kabwe, lilipotajwa, moja kwa moja, watu walimtafsiri kuwa adui wa mageuzi, kwamba yeye ndiye aliyehongwa ili kuhujumu na kudumaza upinzani.

Zitto, akiwa Chadema, Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alitajwa kuwa kwenye mkakati wa kukiangamiza chama hicho. Siasa za kushughulikiana Chadema, zilitua na kutuama kwenye kichwa cha Zitto. Kila jina baya lilielekezwa kwake; kibaraka, msaliti, Yuda. Unaweza kuongeza mengine unayoyajua.

Ukafika wakati, aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, Dk Willibrod Slaa, alikinzana na msimamo wa chama hicho, kuhusu kumpokea Waziri Mkuu wa nane wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Lowassa, na kumfanya kuwa mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2025. Slaa alishughulikiwa hasa. Aliambiwa alinunuliwa ili kuihujumu Chadema.

Ni sawa na Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Cuf. Mgogoro wa kiuongozi dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Seif Sharif Hamad, moja kwa moja, Lipumba alishughulikiwa kila upande, kwamba alihongwa ili kuisambaratisha Cuf.

Kwa sasa, mzunguko upo kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Kila shutuma inaelekezwa kwake, akitajwa kwamba amepokea fedha ili kudhoofisha Chadema. Anatuhumiwa kuwa nyuma ya kile kinachoitwa ni “mradi wa Chaumma”.

Wanamtabiria kuwa ndiye atasimama kama mgombea urais wa Chaumma, katika Uchaguzi Mkuu 2025. Anazodolewa kila mahali picha yake itawekwa mtandaoni. Mbowe, kiongozi aliyebeba maono ya Chadema, na kuitwa majina mengi yenye kumtukuza. Leo amegeuka jalala, lenye kudondoshewa kila takataka.

Ukweli ni kuwa Mbowe analipa gharama ya siasa za kushughulikiana. Mzunguko upo kichwani kwake. Ni aina ya siasa ambazo Chadema wanazipenda. Utazipenda endapo atashughulikiwa mwingine, hasa akiwa hasimu wako. Utaomba ardhi ipasuke utumbukie, inapokuwa zamu yako kushughulikiwa.

Mbowe alikuwa kwenye kivuli, wakati Slaa, Zitto na wengine wengi, wakichomwa na jua kali la kisiasa. Shida ni kwamba, siasa za kushughulikiana, zipo kama mzunguko wa dunia, upo wakati utakuwa gizani, lakini kama wewe ni mhusika wa sayari, basi mwanga utakufikia tu.

Ni siasa za kutajana majina na kuaibishana, zilizomfanya Mbowe, wakati wa sakata la mtakaba wa bandari za Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai, achepuke mada, juu ya faida au hasara za mkataba, moja kwa moja, aliwaelekea Rais Samia na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

Mbowe alihoji, kwa nini Rais Samia na Profesa Mbarawa, wote ni Wazanzibari, lakini mkataba umehusu bandari za Tanganyika peke yake? Hoja ya Mbowe haikubeba ladha nzuri kiuongozi. Badala ya kushughulika na muktadha, Mbowe alishughulika na watu pamoja na maeneo wanayotoka.

Dk Samia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbarawa ni Waziri, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mjadala wowote ambao unahama kutoka muktadha, hadi kushughulika na wajihi au mahali mtu atokako, ni kukengeuka.

Hivi karibuni, Mbowe alihudhuria shughuli ya uzinduzi wa kitabu cha “Dira 2050”. Ni dira ya taifa kwa miaka 25 ijayo. Kwa kupenda au kutopenda, Dira 2050, ilipaswa na inapaswa, kufuatiliwa na kila Mtanzania, awe upande wa upinzani au anayefungamana na Serikali.

Mbowe, alitoa maoni yake kuhusu dira, akakosoa jinsi ambavyo imeandikwa kwamba hakujawa matatizo ya kisiasa na demokrasia. Baadaye, waandishi wa habari, walimtaka Mbowe atoe maoni yake kuhusu msimamo wa Chadema wa “No Reforms, No Election” – “Bila Mabadiliko ya Kikatiba na Kisheria, Hakuna Uchaguzim.”

Akijibu, Mbowe alisema: “Mimi ni mwanachama wa kawaida, msimamo mnatakiwa kuwauliza viongozi. Na viongozi wameshatoa msimamo na unafahamika.” Halikuwa jibu baya. Maana, amesema yeye hawezi kutoa maoni tofauti na msimamo uliotolewa na viongozi.

Hata hivyo, kwa kuwa Mbowe anafuatiliwa ili ashughulikiwe, jibu hilo alilotoa limeibua nongwa. Wana-Chadema wanataka Mbowe angesema kwa kishindo kuwa bila mabadiliko ya Katiba na sheria za uchaguzi, hakutakuwa na uchaguzi. Eti, angesema hivyo, ndiyo angeonekana bado yupo kundini.

Yote yanatokea kwa sababu kwa sasa Mbowe ndiye shabaha ya mashambulizi ya kisiasa. Ndiye anayeonekana adui wa upinzani. Anatwezwa na kuzodolewa bila heshima mitandaoni. Yote hayo ni matokeo ya tabia ya siasa za nchi, kutajana majina na kuaibishana, badala ya hoja za masuala muhimu.