NIKWAMBIE MAMA: Shetani akiporwa kiti hatulii

Niliwahi kusikia na kusoma hadithi za kimila na Maandiko Matakatifu mambo yanayofanana. Shetani, jini au ruhani anapomwingia mtu humfanya kuwa jimbo lake (kiti).

Mwathirika anaweza asione tofauti, lakini wale waliomzunguka huona shaka juu ya mwenendo wa ndugu yao. Watamtafuta mganga na kumpunga shetani huyo. Kwenye maandiko ni vivyo hivyo ila shetani hukemewa na watumishi wa Mungu.

Baada ya kung’atuliwa kitini mwake, shetani huenda kulalamika kwa wakubwa wake. Watamsaidia kwa kumpa mashetani wengine wenye nguvu ya kulikomboa jimbo hilo. Kwa kuwa jambo hili linajulikana na wapinzani wa shetani, mganga ataongeza kinga na watumishi wataongeza maombi.

Hebu ifikirie vita itakayolipuka hapo, zingatia kuwa shetani aliyajua haya ndio maana akaongeza wapambe. Nakiri kuwa nimekuchanganya sana kwa jinsi nilivyoanza stori yangu.

Mwanzoni unaweza kudhani namzungumzia shetani huyu kwenye nafasi ya mbunge anayenyang’anywa jimbo, wakubwa zake kama kamati za siasa na wapambe wake kama wapigadebe kwenye kampeni na kadhalika.

Lakini sipo huko kabisa japo kwenye hitimisho, haya mambo yanafanana. Kwanza tuanze na yetu. Msimu huu chama tawala kimekusanya zaidi ya Sh3.5 bilioni kutoka kwa watiania waliochukua na kurudisha fomu za kugombea uongozi kupitia chama hicho.

Hii ni rekodi kwa Tanzania kupata watu wengi wenye nia ya kugombea udiwani, ubunge na uwakilishi katika kinyang’anyiro cha kupata fursa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Katibu mwenezi wa chama hicho amenadi kuwa huo ni ukomavu wa kidemokrasia kwani kwani kuchukua fomu ni haki ya kila anayekidhi vigezo.

Lakini ni lazima tukubaliane na ukweli kwamba kinachohitajika ni ubora na sio wingi wa watiania.

Wanaohakiki ubora ni kamati zilizomo ndani ya chama, hapa nawafananisha na wahudumu wanaotuandalia chakula. Sisi wapigakura ni sawa na walaji tunaoletewa jamvini. Tunawatazama watiania katika makundi mawili.

Wapo ambao wamezoeleka kuonekana katika shughuli za kila siku za chama na hakuna anayeweza kutia neno akisikia wanataka uongozi. Kundi la pili, ni watia nia wapya ambao hawana historia ya kujishughulisha na chama. Baadhi yao ni wanamapinduzi wenye nia ya kurekebisha mapungufu yaliyosababishwa na viongozi waliotangulia.

Katika makundi yote mawili wamo watu wanaotofautiana. Kundi la kwanza lina viongozi waadilifu waliokuzwa katika zama za Ujamaa na Kujitegemea.

Hawa hutaniwa kuwa “wamekunywa maji ya bendera.” Ni viongozi waadilifu wasioamini katika rushwa na ubadhirifu. Lakini hawapati sifa nyingi kwani ni waoga wa kuongea hadharani au kwenye vyombo vya habari kwa kuogopa “kuteleza.”

Lakini humuhumu wapo wale wasiotaka mabadiliko. Wanaoishi kwa propaganda za siasa zaidi kuliko uhalisia ulivyo.

Wengi wao wanapinga kuondoka kwenye viti vyao kwa kuogopa madudu yao yasianikwe hadharani, au kwa kuogopa kuutia kutu mnyororo wao.

Nyuma yao kuna mnyororo mrefu unaowahusisha hadi viongozi wa ngazi za juu, ni wakonsevativu walio tayari kuishi na makosa ya kundi lao.

Cha ajabu ni kwamba kwenye kundi hili pia kuna wanaopepea kama bendera. Wanayakubali sana mawazo ya viongozi wapya, lakini hawapo tayari kusimama hadharani na kuwaunga mkono.

Huu ni woga wa kuonekana wasaliti mbele ya waliowasaidia kufika hapo walipo. Wenye mioyo migumu wanaweza kufikia hatua ya kung’atuka kisiasa na kubaki kuwa raia watiifu huku mitaani.

Kundi jipya lina vijana wengi wasioamini uongozi wa mazoea.

Hiki ni kizazi cha sayansi na teknolojia kinachoamini kuligeuza Taifa kwa njia za kisayansi. Wengi wanazisoma siasa za kiulimwengu, na wanayaona humo mabadiliko ya siasa za Tanzania.

Wana maono mazuri lakini hawakubaliki kwa asilimia nyingi na Kamati za chama zinazochuja watiania.

Kila kundi lina ubora na udhaifu wake. Hawa hawasikilizi matatizo ya wananchi, wanaidumaza nchi na wanasigina haki za binadamu.

Lakini wale wanaweza kutusikiliza ila wanaweza pia kutuingiza matatani. Neno “haki za binadamu” linapenya masikioni kwa urahisi sana, lakini tafsiri yake ni mtambuka. Mnaweza kujikuta mkishtakiwa na mashoga kwa kuwakatalia usajili. Tunawataka viongozi wenye uwezo wa kuachana na mazoea. Hakuna siku ambayo bajeti ilionesha kuwa Tanzania imeondokana na utegemezi.

Inamaanisha watanzania hawajawahi kuwa na hali bora hata siku moja! Kama ilitokea basi ni nyakati zile kabla ya utumwa na ukoloni. Je, tumeumbwa tuwe hivyo? Sasa basi kwa nini tunapambana kujikwamua? Watanzania wamechoshwa na ufukara uliokithiri.

Waliwahi kuyakataa masharti ya Shirika la Fedha Duniani na Benki ya Dunia kwa sababu yalituingiza mkengeni. Ili kupata viongozi wakweli vyama vitengeneze sera na dira zinazotokana na mila na tamaduni zetu.

Machifu wetu walikuwa imara kwa kuwa walizilinda na kuzienzi mila zao. Ingawaje kwa sasa jambo hili ni gumu kutokana na utandawazi, lakini vyama vitusaidie kuwapata wagombea wasiouonea aibu uzalendo. Wachina na Wahindi waliukataa utumwa na kuenzi mila zao, sasa wanashereheka kichina na Kihindi.