UONGOZI wa Pamba Jiji umemalizana na kocha Mkenya Francis Baraza kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili akipishana na Fredy Felix ‘Minziro’ aliyepambana kuibakisha timu hiyo.
Baraza ana uzoefu wa soka la Tanzania, kwani amepita Biashara United na Kagera Sugar anatarajia kuwasili nchini Agosti Mosi tayari ya kuanza majukumu ya kuiweka tayari timu hiyo kwa mchaka mchaka wa msimu wa 2025/26.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zimebainisha tayari Pamba imemalizana na kocha huyo kwa mkataba wa miaka miwili na kumtaarifu anatakiwa kuwa Tanzania mapema Agosti Mosi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
“Tumefanikisha mpango wa kumnasa Baraza kama ambavyo mipango ilikuwa, sasa ni kufahamu ni namna gani tunajipanga kuhakikisha tunakuwa bora na hatufanyi makosa kwa kujiweka kwenye presha kama ilivyokuwa msimu ulioisha,” kilisema chanzo hicho.
Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta Baraza aliyepo Kenya, naye alikiri kufanya mazungumzo na Pamba Jiji japo hayupo kwenye nafasi nzuri ya kuzungumzia walipofikia anauacha uongozi wa timu hiyo kuweka wazi hilo.
Baraza mbali na kuzifundisha Biashara United na Kagera Sugar, pia amezifundisha Polisi Kenya, Tusker, Chemelil Sugar, Western Stima na Sony Sugar za huko Kenya.
Minziro aliyezifundisha timu mbalimbali zikiwemo za Geita Gold na Tanzania Prisons, alijiunga na Pamba Oktoba 17, 2024, ili kuchukua nafasi ya Mserbia Goran Kopunovic, aliyeanza nayo msimu kisha kuondoka Oktoba 16, 2024.
Pamba iliyorejea Ligi Kuu Bara 2024-2025 baada ya kupita miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, imemaliza msimu wa 2024-2025, ikiwa nafasi ya 11 na pointi zake 34, ikishinda mechi nane, sare 10 na kupoteza 12, kati ya 30, ilizocheza.