Ngoma imekuwa ngumu. Ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya kukwama kwa dili la Tanzania Prisons kumvuta Ahmad Ally kutua kikosini humo kwa ajili ya msimu ujao na kuamua kukimbilia nchini Kenya kumchukua Zedekiah Otieno kuwa kocha mkuu wa timu hiyo.
Iko hivi, Wajelajela hao walikuwa na hesabu za makocha watatu, Ahmad Ally wa JKT Tanzania, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ na Patrick Odhiambo ili mmoja wapo aweze kuungana na maafande hao.
Vigogo wa timu hiyo waliamua kumvutia simu kocha Ally kwa ajili ya kuvunja mkataba wake pale JKT Tanzania lakini unaambiwa dau alilotaka kocha huyo na masharti aliyowapa, Tanzania Prisons imeamua kunyoosha mikono na kumchukua mwingine.
Habari za kuaminika kutoka kwa Maafande hao ni kuwa, baada ya kumkosa Ally ambaye ndiye alibaki peke yake kati ya majina matatu yaliyokuwepo mezani awali, wameamua kutua nchini Kenya na kumshusha Otieno aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa hilo, ‘Harambee Stars’.
Taarifa zinaeleza kuwa, uamuzi wa kumchukua Otieno ni baada ya kocha huyo wa zamani wa Gor Mahia jina lake kuwasilishwa mezani na kujadiliwa kisha kupitishwa.
Baada ya kufikia makubaliano ya awali, kocha huyo tayari amewasili Dar es Salaam kwa ndege leo asubuhi na anatarajia kuelekea yalipo makao makuu ya timu hiyo, Dodoma kwa ajili ya kutambulishwa kisha kuelekea Mbeya kwa ajili ya kuanza majukumu.
“Dili la makocha hao waliokuwa wakipigiwa hesabu wote mambo yamegoma na sasa tunamsubiri huyu kocha kutoka Kenya akutane na viongozi leo kwa ajili ya kutambulishwa kisha kupewa maelekezo ya kazi.
“Kocha Ally ndiye alikuwa chaguo zaidi lakini gharama yake imekuwa kubwa kuliko uwezo wa timu, tumeamua kufanya vinginevyo na matarajio ni kupata matokeo mazuri,” kimesema chanzo ndani ya kikosi hicho.
Chanzo hicho kilifichua moja ya sharti alilowapa Ally ili kutua Tanzania Prisons ni kupatiwa mshahara wa Sh12 milioni kwa mwezi nje ya posho, huku pia atue kikosini hapo na wasaidizi wake wawili ambao kila mmoja atalipwa Sh4 milioni.
Kuhusu usajili wa nani kaingia nani katoka, chanzo hicho kimesema bado kikao kinaendelea na leo huenda wakaanza kupendekeza majina ya nyota wapya kwa kuwa lazima manadiliko yawepo.
“Kikao kimeanza jana na leo huenda tukamaliza, kwa kuwa kocha amepatikana tunaanza kupendekeza wachezaji, kikubwa tunahitaji kikosi chenye ushindani kutupa matokeo mazuri, uongozi uko imara,” kimesema chanzo hicho.