Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Hayati Benjamin Mkapa atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi cha sasa na kijacho kutokana na mchango wake mkubwa katika kujenga misingi ya maendeleo, utawala bora na ustawi wa Taifa.
Amesema Serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na Mkapa ilijenga nguzo muhimu za umoja wa kitaifa, Muungano, amani na mshikamano wa Watanzania, pamoja na nafasi ya Tanzania katika bara la Afrika na ulimwenguni.
Rais Mwinyi ameyasema hayo leo Jumatano, Julai 23, 2025 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, katika Ibada Maalumu ya Kumbukumbu ya miaka mitano ya kifo cha Mkapa iliyofanyika Lupaso, Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara.
Mkapa alifariki dunia usiku wa Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam akiwa na miaka 81 baada ya kuugua ghafla. Mwili wake, ulizikwa Lupaso.

Aidha, Rais Mwinyi amekumbusha kuwa Hayati Mkapa alikuwa muumini wa ujamaa na uchumi wa soko unaoongozwa na sekta binafsi, lakini alihakikisha maendeleo yanawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.
Amesema Hayati Mkapa ndiye aliyeanzisha Dira ya Maendeleo 2025, ambayo imekuwa chombo muhimu katika mageuzi ya maendeleo na mafanikio yake yamekuwa msingi wa kuzinduliwa kwa Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Halikadhalika, Rais Mwinyi ametoa wito kwa viongozi wa dini, wanasiasa na wanahabari kuwa sehemu ya kulinda na kuendeleza tunu ya amani kama njia ya kumuenzi Hayati Mkapa.
Amesema Watanzania wanayo sababu ya kujivunia viongozi waliopo ambao wanaendeleza maono ya viongozi waasisi na kuipeleka Tanzania mbele katika nyanja zote za maendeleo.

Rais Mwinyi alizuru kaburi la Hayati Mkapa na kuweka shada la maua, akiongozana na Rais mstaafu wa Msumbiji, Filipe Nyusi na mkewe pamoja na Mjane wa Hayati Mkapa, Mama Anna Mkapa.