RAIS MWINYI: HAYATI MZEE BENJAMIN WILLIAM MKAPA NI MFANO WA KUIGWA KWA MCHANGO WAKE KWA TAIFA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuwa Hayati Mzee Mkapa atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi cha sasa na kijacho kutokana na mchango wake mkubwa katika kujenga misingi ya maendeleo, utawala bora na ustawi wa Taifa. 

Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijenga nguzo muhimu za umoja wa kitaifa, Muungano, amani na mshikamano wa Watanzania, pamoja na nafasi ya Tanzania katika bara la Afrika na ulimwenguni.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ibada Maalum ya Kumbukumbu ya Miaka Mitano ya Hayati Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyofanyika leo tarehe 23 Julai 2025 Lupaso, Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amekumbusha kuwa Hayati Mzee Mkapa alikuwa muumini wa ujamaa na uchumi wa soko unaoongozwa na sekta binafsi, lakini pia alihakikisha kuwa maendeleo yanawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi. 

Ameeleza kuwa Hayati Mzee Mkapa ndiye aliyeanzisha Dira ya Maendeleo 2025, ambayo imekuwa chombo muhimu katika mageuzi ya maendeleo, na mafanikio yake yamekuwa msingi wa kuzinduliwa kwa Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa viongozi wa dini, wanasiasa na wanahabari kuwa sehemu ya kulinda na kuendeleza tunu ya amani kama njia ya kumuenzi Hayati Mkapa. 

Amesema kuwa Watanzania wanayo sababu ya kujivunia viongozi waliopo ambao wanaendeleza maono ya viongozi waasisi na kuipeleka Tanzania mbele katika nyanja zote za maendeleo.

Rais Dkt. Mwinyi alizuru kaburi la Hayati Benjamin William Mkapa na kuweka shada la maua, akiongozana na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi, na Mkewe pamoja na Mjane wa Hayati Mkapa, Mama Anna Mkapa. 

Hayati Mzee Mkapa alifariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 24 Julai 2020 akiwa na umri wa miaka 81, jijini Dar es Salaam.