RC ARUSHA AWATAKA POLISI KUTOGEUZA BODABODA CHANZO CHA MAPATO

Na Seif Mangwangi, Arusha

MKUU wa Mkoa wa Arusha Kenan Kihongosi ametoa siku tatu kwa madereva wa bodaboda Mkoa wa Arusha kuondoa kelele maarufu kama ‘Mafataki’ kwenye pikipiki zao kwa kuwa zimekuwa zikisababisha maradhi na kustua wagonjwa.

Aidha Kihongosi amewataka Askari wa usalama barabarani Mkoani humo kutowageuza madereva wa bodaboda kama chanzo cha mapato kwa kuwapiga faini kila wakati.

“Nikiwa Mkoa wa Arusha nitalinda haki zenu, Askari naomba msigeuze bajaji na pikipiki kama chanzo cha mapato, ikitokea kila kosa mnawapiga faini watakuwa maskini, wameamua kujiajiri tuwasaidie kwa kuwalea, kaeni nao na kuzungumza nao, ” amesema Kihongosi alipokuwa akizungumza na madereva wa bodaboda, guta na bajaji Mkoa wa Arusha jana Julai 22, 2025.

Amesema bodaboda wakishindwa kulipa rejesho watarudi mtaani na kusababisha madhara mengi ikiwemo kurejea kwenye ukabaji kwa wale waliokuwa wakifanya kazi hiyo kabla ya kuacha jambo ambalo litahatarisha maisha yao.

“Mimi nilikuwa dereva bodaboda kwa miaka minne, najua faida yake na utundu mwingi pia nimefanya, sasa nawambeni muache michezo ya mafataki, nawapa siku tatu, wale walioharibu exhost waende wakarekebishe baada ya hapo ukikamatwa hatutakusamehe,” aliagiza.

Aidha madereva wa vyombo hivyo wamemuomba Mkuu wa Mkoa kuwaongezea maeneo ya maegesho wakidai kuwa maeneo waliyotengewa yamekuwa machache kutokana na wingi wa vyombo hivyo.

Akiwasilisha risala ya waendesha bodaboda, katibu wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Mkoa wa Arusha, Hakimu Msemo amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa baadhi ya madereva wa bodaboda hawana leseni za udereva hali inayochangia ajali.

Msemo alimtaka Mkuu wa Mkoa kutoa tamko kali dhidi ya madereva wanaofanya kazi bila leseni kwani hali hiyo si tu inaleta hatari kwa abiria bali pia inatishia hadhi ya sekta hiyo.

“Hapa Arusha tupo bodaboda zaidi ya elfu 24 lakini changamoto kubwa wengi hawana elimu ya udereva hivyo tunaomba utoe kauli dhidi yao, lakini pia tunaomba wapatiwe mafunzo ya udereva kwani wao ndiyo chanzo kikubwa cha ajali” alisema.

Kwa upande wao madereva wa Bajaji Mkoa wa Arusha kupitia kwa Katibu wao, Salim Lyimo alisema kuwa maeneo waliyopewa yapo mbali na mji, masoko, hospitali na hoteli za kitalii hivyo kuathiri moja kwa moja idadi ya wateja wao.

“Makadirio ya bajaji zilizopo ni zaidi ya 3,500 huku vituo vikiwa ni changamoto kubwa, hivyo tunaomba tupatiwe maeneo mazuri na tunashauri wenye leseni, makundi maalum pamoja na wenye ulemavu wapatiwe kipaumbele” alisema Lyimo.

Akijibu maombi ya madereva hao, Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa vyombo vyote vya usafiri na wasafirishaji kuhakikisha wanazingatia sheria, wanapata leseni na wanashirikiana na serikali kuifanya Arusha iwe safi, salama na ya kuvutia.

Alisema serikali ipo tayari kuwasikiliza wananchi lakini lazima kila upande uwe tayari kwa mabadiliko ya maendeleo.

“Lazima tutafute njia bora ya kupungumza msongamano, lakini niwaambie ukweli kuhusu ombi lenu la kutafutiwa maegesho katika maeneo mliyoyataja kuwa naenda kulifanyia kazi, nitakaa na wataalamu wangu, kama linawezekani nitawaita hapa hapa na kuwaeleza,” alisema Kihongosi.