RC KIHONGOSI ASIKILIZA KERO ZA WANANCHI WILAYA ARUMERU.

Na Veronica Ignatus 

Mkuu wa mkoa wa Arusha Kenan Kihongosi  amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Arumeru kuwa changamoto zao zitatuliwa kwa wakati lengo ni kila mmoja kuona matunda ya kazi inayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Amesema ameletwa katika mkoa huo ili kwa ushirikiano wa pamoja waweze kuleta mabadiliko ya uchumi wa kila mmoja na taifa kwa ujumla.

Katika changamoto zilizotolewa na wananchi zimepatiwa majibu ya awali na Watendaji wanaohusika tayari wameanza kushughulikia chagamoto zao. 

Kihongosi amesema lengo la kufanya hivyo ni kuona ustawi wa wananchi unaimarika, kufanya kazi katika mazingira rafiki na kustawisha amani ya nchi. 

Pia amesisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo Oktoba 25 mwaka huu. Amewaasa kutosikiliza watu wchache wanaosema uchaguzi hautafanyika mwaka huu. 

Amesema”tuilinde amani ya nchi yetu kila mmoja kwa nafasi yake, tusidanganywe na watu wachache ambao watoto wao wanaishi na kusoma nje ya nchi, ndio maana wanachochea maandamano na vurugu katika nchi yetu”, 

“Ni dhahiri kwamba Tanzania ya leo sio ile ya miaka kumi iliyopita, mabadiliko ni makubwa na maendeleo yanaonekana, tulinde amani yetu na kujenga mshikamano katika kulijenga taifa letu” amesema Kihongosi.

Kihongosi ametoa agizo kufanyika kwa operesheni kuhakikisha yeyote anayejihusisha na biashara ya gongo anachukuliwa hatua kali.