Klabu ya Yanga imemtambulisha Romain Folz kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa 2025-2026.
Kocha huyo mwenye leseni ya UEFA Pro na CONBEL Pro, ametua Yanga kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Miloud Hamdi aliyetimkia Ismailia ya Misri baada ya kudumu kwa takribani miezi sita na kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Muungano na Kombe la FA.
Kabla ya Yanga kumtambulisha kocha huyo, Mwanaspoti lilikuhabarisha juu ya ujio wake kumrithi Hamdi.
Rekodi zinaonesha Romain Folz licha ya umri wake mdogo wa miaka 35 alionao, lakini ni kocha mzoefu aliyehudumu katika klabu mbalimbali huku akiwa analifahamu vizuri soka la Afrika kutokana na kufundisha timu kadhaa za bara hili.
Mzaliwa huyo wa Bordeaux nchini Ufaransa, safari yake ya ukocha ilianza rasmi mwaka 2018 alipoteuliwa kuwa kocha mkuu wa klabu ya West Virginia United nchini Marekani.
Mwaka 2019, alihudumu kama kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uganda. Baada ya hapo, aliteuliwa kuwa kocha msaidizi wa klabu ya Pyramids nchini Misri.
Mwaka 2020, Folz aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa klabu ya Bechem United ya Ghana. Kisha alihamia Ufaransa kuwa kocha msaidizi wa klabu ya Niort.
Mwaka 2021, alikabidhiwa mikoba ya kuinoa klabu ya Ashanti Gold ya Ghana, kabla ya kwenda Botswana kuifundisha klabu ya Township Rollers.
Mwaka 2022, alihamia Afrika Kusini kwa mara ya kwanza na kuifundisha Marumo Gallants, akiwa ndiye kocha mdogo zaidi katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini. Aliongoza klabu ya AmaZulu kuanzia mwaka 2022 hadi 2023, ambapo mwezi Aprili 2023 alihamishiwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi.
Mnamo Agosti 2023, alijiunga na klabu ya Horoya AC ya Guinea. Kisha mwezi Julai 2024 alijiunga na Mamelodi Sundowns F.C. ya Afrika Kusini kama kocha msaidizi hadi tarehe 10 Desemba 2024.
Machi 2025 alitua klabu ya Olympique Akbou inayishiriki Ligi Kuu ya Algeria akiwa Mkurugenzi wa Michezo, nafasi ambayo aliitumikia hadi Julai 2025, kisha ametua Yanga.
Mtihani wa kwanza alionao Folz ni kutetea taji la Ngao ya Jamii 2025, kisha kuiongoza Yanga kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2025-2026.
Pia Mfaransa huyo atatakiwa kutetea mataji mengine iliyoshinda Yanga msimu wa 2024-2025 ambayo ni Kombe la Muungano na Kombe la FA.