Sekta ya madini inavyodahili wanafunzi wachache vyuoni

Dar es Salaam.  Ripoti zinaonesha mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa unaendelea kukua.

Mwaka 2024, sekta hiyo ilichangia asilimia 10.1 ya Pato la Taifa, ikilinganishwa na asilimia 7.1 mwaka 2021 ikiwa tayari imepita lengo la asilimia 10 la mwaka 2025.

Sekta hii imeendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, huku Serikali ikiimarisha sera na mifumo ya usimamizi wa rasilimali hizo muhimu.

Hata hivyo, mafanikio haya hayawezi kuwa endelevu bila kuwekeza kwa makusudi katika rasilimali watu, kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya sekta hiyo inayohitaji wataalamu waliobobea katika maeneo kama jiolojia, uhandisi wa migodi, usalama kazini, mazingira, uchambuzi wa kisera, pamoja na biashara na fedha.

Uwekezaji katika mafunzo ya kitaaluma na ya vitendo huongeza ufanisi, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa zinazohitajika kwa uchimbaji endelevu na wa thamani zaidi.

Pia, uwekezaji huu huongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo, kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje na kukuza ajira zenye staha kwa vijana.

Haya yanaonekana wakati ambao takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) zinaonesha madini na sayansi ya dunia ndiyo fani inayoongoza kwa kuwa na idadi ndogo ya watu wanaodahiliwa vyuoni kwa miaka minne mfululizo huku wadau wakitoa mbinu za kuongeza idadi hiyo.

Katika mwaka wa masomo 2024/25, ni wanafunzi 604 pekee ndiyo waliodahiliwa kusoma madini na sayansi ya dunia (Mining and earth science) ikiwa ni ongezeko kutoka 570 waliokuwapo mwaka 2021/22.

Idadi ya wanafunzi iliyokuwapo mwaka 2021/22 ilipungua hadi kufikia 421 mwaka 2022/23 kabla ya kuongezeka kufikia 589 mwaka 2023/24.

Licha ya kuwapo kwa ongezeko hilo la takribani asilimia sita  katika kipindi cha miaka minne lakini bado fani hiyo ndiyo inayoendelea kushuhudia udahili mdogo kwa miaka yote mfululizo.

Mtaalamu wa Biashara na uchumi, Dk Donath Olomi amesema kutozalishwa kwa wataalamu wa kutosha, sekta ya madini itashindwa kukua kwa kiwango kikubwa zaidi (ikijiminya) kutokana na kukosa watu wanaoweza kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ikiwamo utafiti, ushauri, ujenzi, uchakataji.

Hali hiyo itaifanya nchi kutumia wataalamu kutoka nje ya nchi au wale wasiokuwa na utaalamu unaohitajika hali itakayofanya sekta kujikongoja.

“Lakini hata hawa waliosoma tuangalie wamejifunzaje, wasiwe wamesoma madini kwa nadharia na hawana ujuzi unaotakiwa, ni vyema sana kufanya uchambuzi wa uhitaji katika sekta na mnyororo mzima wa thamani wa madini aina mbalimbali; hiyo itatoa jibu kuwa tunahitaji kusomesha watu wa aina gani wanaohitajika sokoni,” amesema Dk Olomi.

Amesema ili kuwa na watu wengi wanaosoma kozi hiyo, ni vyema nchi kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi kwa kile alichosema kuwa, kwa sasa kuna shida ya walimu hasa katika masomo ya hesabu, fiziki na kemia.

Dk Olomi amesema uwepo wa wataalamu hao unaweza kusaidia kuboresha uchimbaji kutoka watu kutumia nyenzo duni na njia zisizo rasmi hali inayofanya tija kutokuonekana kwa kiasi kikubwa.

“Inaweza kusaidia kuwa na watu wanaofanya kazi kwa tija wakitumia njia za kisasa zaidi,” amesema Dk Olomi.

Katika kujenga ushirikishwaji wa wazawa katika sekta hiyo, amesema rasilimali watu ni sehemu muhimu inayohitajika ambayo itaenda sambamba na utengenezaji wa mazingira wezeshi, ili Watanzania washiriki katika uchakataji, uchimbaji na uongezaji thamani madini.

Bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kupitia bajeti yake ya mwaka 2025/2026 inaeleza katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2020 walimu 106,806 wamepewa mafunzo wakiwamo  29,399 wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknolojia kwa lengo la kuimarisha ufundishaji wa masomo hayo

“Hali hii imefanya idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi na Hisabati katika shule za sekondari kuanzia kidato cha tatu imeongezeka kutoka 2,497,450 hadi 2,792,584 sawa na ongezeko la wanafunzi 295,134,” alisema Mohammed Mchengerwa ambaye ni waziri anayesimamia wizara hiyo alipokuwa akiwasilisha bungeni bajeti.

Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude amesema kama unataka kuingiza watu wengi katika sekta husika ni lazima kutengeneza nafasi nyingi za ajira ili watu waweze kuona umuhimu wa kusoma fani husika katika ngazi mbalimbali.

Hiyo ni kwa sababu sasa hivi kabla ya kuchagua fani za kusoma vijana wamekuwa wajanja kuangalia kile wanachokichukua watakwenda kukifanyia kazi katika maeneo gani tofauti na ile sekta kusudiwa.

“Tunaweza kufungua upande wa ajira kwanza ili kuvuta watu wengi, kwa kuanzia tunaweza kufungua hizo nafasi na tukiwa hatuna wataalamu wa kutosha tukaacha ichukuliwe na hata watu wa nje kama Kenya, Uganda lakini tukijua baada ya muda tutawatoa wote na sisi kukaa hapo,” amesema.

Amesema ili kufanikisha hilo ni vyema kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu kwa kuwekewa mazingira mazuri.

Katika kufungua fursa upande wa madini amesema mchakato wa uanzishaji sehemu za uongezaji thamani ufanyike kwa haraka ili kuhakikisha vijana wanaomaliza vyuo wanaweza kuajiriwa jambo litakaloongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta.

Hata hivyo, amesema kwa ufinyu wa migodi iliyopo nchini, idadi ya wanafunzi 604 wanaodahiliwa ni kubwa kwa kuwa, kwa sasa ni ngumu wote kuajiriwa kutokana na teknolojia kutumika kwa kiasi kikubwa.