Serikali yasuka mkakati kuwarudisha wanafunzi wanaoacha shule Geita

Geita. Zaidi ya wanafunzi 2,500 wa shule za sekondari katika Manispaa ya Geita wamekatisha masomo ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita, chanzo kikuu kikiwa ni utoro.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba ameiagiza manispaa hiyo kufanya tathmini ya kina kubaini walipo watoto hao, ili waweze kurejeshwa shuleni kupitia programu maalumu ya Serikali ya kuwaendeleza kielimu.

Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba akizungumza wakati wa kufunga mashindano ya michezo kwa wanafunzi wa shule za Sekondari Manispaa ya Geita

Akizungumza wakati wa kufunga mashindano ya michezo kwa shule za sekondari yaliyoendeshwa chini ya kaulimbiu “Tukutane Shuleni, Tujenge Kesho Iliyo Bora” na kudhaminiwa na Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu Geita (GGML), Komba amesema ongezeko la mdondoko wa wanafunzi linatia wasiwasi na linahitaji hatua za haraka kukabiliana nalo.

“Takwimu hizi zinashtua. Swali ni je, watoto hawa wamekwenda wapi? Fanyeni tathmini kwa kushirikiana na watendaji wa mitaa mjue walipo,” amesema Komba.

Komba ameongeza kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, Taifa linaweza kuingia kwenye hatari ya kulea kizazi tegemezi, kilicho katika hatari ya kujiingiza kwenye makundi ya uhalifu mimba za utotoni na maamuzi hatarishi ya maisha.

Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Geita, Rashid Muhaya amesema tatizo la mdondoko linachangiwa kwa kiasi kikubwa na utoro wa wanafunzi.

Kwa mujibu wa takwimu, mwaka 2021 wanafunzi 916 waliacha shule (wavulana 428, wasichana 488), mwaka 2022 walikuwa 872 (wavulana 463, wasichana 409) na mwaka 2023 walikuwa 759 (wavulana 397, wasichana 362).

Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba akizungumza wakati wa kufunga mashindano ya michezo kwa wanafunzi wa shule za Sekondari Manispaa ya Geita

Amesema, ili kukabiliana na hali hiyo, manispaa ilianzisha mashindano ya michezo kwa shule za sekondari kama mkakati wa kuhamasisha wanafunzi kubaki shuleni na kuwavutia waliokatisha masomo kurejea.

“Michezo imetumika kama njia ya kuwarudisha wanafunzi shuleni, kuongeza mahudhurio, na kudhibiti utoro. Pia, ni fursa ya kuibua vipaji, kuimarisha mshikamano baina ya wanafunzi na walimu, na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu,” amesema Muhaya.

Mashindano hayo pia yamebeba ujumbe wa kuhimiza jamii kuchangia chakula shuleni, kuwakinga watoto dhidi ya mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia, pamoja na kujenga nidhamu kwa vijana.

Mwakilishi wa GGML, Charles Masubi amesema kampuni yao iliona ni muhimu kushirikiana na manispaa kutokana na athari kubwa za mdondoko wa wanafunzi.

“Mashindano haya yamekuwa zaidi ya michezo. Yamekuwa jukwaa la kutoa ujumbe muhimu juu ya changamoto ya mdondoko. Kila kijana anayekatisha masomo ni ndoto iliyovunjika na ni hasara kwa mustakabali wa Geita na Taifa kwa ujumla,” amesema Masubi.

Ameongeza kuwa michezo, inapowekwa kwenye mazingira bora, ina uwezo wa kuhamasisha, kuelimisha, na kubadili maisha ya vijana, ikiwapa moyo wa kurudi shuleni, kujifunza nidhamu, mshikamano na kuamini kuwa kila kitu kinawezekana.