Serikali yatoa kauli sakata la Polepole

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema taarifa kuhusu Balozi Humphrey Polepole zitatolewa mamlaka husika zitakapokamilisha taratibu.

Balozi Polepole aliandika barua ya kujiuzulu Julai 13, 2025, kwenda kwa Rais Samia Suluhu Hassan akitaja sababu ni kutoridhishwa na mwelekeo wa uongozi usiojielekeza katika kusimamia haki, amani na kuheshimu watu.

Barua hiyo ambayo Balozi Polepole aliichapisha katika ukurasa zake za kijamii, imeibua mjadala katika mitandao ya kijamii na baadaye aliitisha mkutano wa waandishi wa habari, akidai anaifafanua.

Balozi Kombo ameyasema hayo leo, Jumatano Julai 23, 2025 alipoulizwa swali wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa 27 wa mawaziri na maofisa waandamizi wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Amesema naye ameona taarifa kama ilivyoonekana na wengine, lakini kwa ilivyoandikwa haikuelekezwa kwake, bali kwa mamlaka nyingine.

Kwa sababu hiyo, amesema inakuwa vigumu kwake kusema lolote, badala yake mamlaka iliyoelekezwa barua husika ndiyo yenye nafasi ya kufanya hivyo.

Hata hivyo, amesema suala la kiongozi huyo linahusisha sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, anaamini zitakapokamilika taarifa itatokewa.

“Suala lile lina masuala ya kisheria, kanuni na masuala ya utumishi wa umma na lina taratibu zake, zikikamilika kwa utumishi wa umma taarifa za kina zitatolewa,” amesema.