Simba ina vyuma vitatu, hivi hapa!

MABOSI wa Simba wanaendelea kufanya usajili wa mastaa wapya kimya kimya, huku tetesi zikisema hivi sasa imefikia makubaliano kamili ya kumsajili kiungo wa kati raia wa Senegal, Alassane Kante (24) kutoka CA Bizertin ya Tunisia, huku kocha wa kikosi hicho Fadlu Davids akiwa kwenye mazungumzo na viungo wengine wawili.

Msenegali huyo ambaye ameitumikia CA Bizertin kwa misimu mitatu mfululizo tangu alipojiunga nayo Oktoba 2022, amekuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi hicho, huku Simba ikiweka kibunda cha maana kumnunua kwani bado alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja.

Rekodi zake zinaonyesha ni kiungo hatari mwenye uwezo mkubwa wa kutawala eneo la katikati na anasifika kwa kuwapa shida wapinzani, pia ni miongoni mwa mastaa waliokuwa wanapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza muda mwingi.

Kante anakwenda kumuongezea nguvu Yusuph Kagoma ambaye msimu uliomalizika alikuwa akicheza nafasi hiyo na Fabrice Ngoma, Debora Mavambo na Augustine Okejepha ambao wote wameshaaga, huku akisalia Mzamiru Yassin lakini mkataba wake nao umekwishamalizika japokuwa hatma yake bado haijajulikana.

Taarifa kutoka Simba zinasema: “Kante anatarajiwa kutua Bongo muda wowote kuanzia sasa ili kukamilisha masuala ya usajili, pia muda wa kwenda pre-season umekaribia, hivyo wachezaji wanaanza kuripoti.

“Wakati wowote mkataba rasmi utasainiwa kwani makubaliano kamili kati ya pande zote yameshafanyika na Simba ilishalipia Dola 285,000 (Sh742 milioni) kumaliza mwaka wa mwisho uliosalia, hivyo akitua Tanzania atapimwa afya kisha masuala mengine yataendelea.”

Ukimweka kando Kante, Kocha Fadlu anataka kuziba nafasi ya viungo watatu wa kimataifa waliiondoka ambao ni Mavambo, Ngoma na Okejepha ambao walikuwa wakipishana katika kucheza au wakati mwingine wakianza wawili pamoja.

Katika mchakato huo, ndipo lilipotua jina la kiungo raia wa Benin, Rodrigue Kossi Fiogbé (25) ambaye amemaliza mkataba wake rasmi msimu uliomalizika na ES Setif ya Algeria.

Taarifa za ndani kutoka Simba zililiambia Mwanaspoti: “Kocha Fadlu kwa sasa ndiye anayefanya usajili wa mastaa wa kigeni kwa msimu ujao na anataka kwenye eneo la katikati awe na viungo watatu, ndiyo maana anapambana kuwapata wawili wa kigeni na mmoja mzawa.

“Simba ina urahisi zaidi kwenye dili la Rodrigue kwa sababu ni mchezaji huru tangu Julai Mosi mwaka huu, hivyo kwa sasa kuna mazungumzo yanaendelea na uongozi wa mchezaji huyo.”

Kama utakuwa unakumbuka vyema, Mwanaspoti iliwahi kuandika kuwa, katika maeneo ambayo ripoti ya kocha Fadlu imelenga ili kuongezewa nguvu msimu ujao ni kiungo mshambuliaji anapocheza mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara 2024-2025, Jean Charles Ahoua.

Uhitaji huo wa Kocha Fadlu ndio maana Simba ilianza harakati za kumsaka Feisal Salum ‘Fei Toto’ lakini ikagonga mwamba kutokana na dau kubwa ililotaka Azam FC, ndipo ilipoanza kusaka jembe jipya.

Harakati hizo zilianza baada ya kocha kuwaambia mabosi Ahoua anahitaji kupata msaidizi kama yeye hatokuwepo kwani alitumika sana msimu uliomalizika alipofunga mabao 16.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, licha ya Simba kuwa kimya, lakini iko kwenye mazungumzo na kiungo mshambuliaji Mkongomani, Charve Onoya Sangana (21) ambaye bado ana mkataba na Union Maniema ya DR Congo.

“Simba ipo kwenye mazungumzo ili kumpata kiungo huyo ambaye atakuwa anacheza kwa kusaidiana na Ahoua kama ripoti ya kocha ilivyohitaji,” kilisema chanzo.

Simba mpaka sasa haijamtangaza mchezaji yoyote mpya zaidi ya kutoa mkono wa kwa heri na wameondoka nyota tisa, wapo waliomaliza mikataba na waliofikia makubaliano ya kutoendelea nao, huku mmoja akitolewa kwa mkopo.

Wachezaji walioagwa rasmi ndani ya Simba ni Aishi Manula, Kelvin Kijili, Valentin Nouma, Hussein Kazi, Mohamed Hussein, Fabrice Ngoma, Debora Mavambo, Augustine Okejepha na Omary Omary ambaye amepelekwa Mashujaa kwa mkopo.