Sowah, Simba ni suala la muda tu, ishu nzima ipo hivi!

SIMBA inaendelea kuimarisha kikosi kimya kimya hii ni baada ya kutajwa kumalizana na Jonathan Sowah kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Singida Black Stars.

Sowah aliyekuwa akihusishwa na Yanga kutokana na ubora wake wa kufumania nyavu na baadae Yanga kukamilisha dili la Celestin Ecua na dili lake la kutua Jangwani likafa rasmi.

Inadaiwa kuwa, Simba  ipo katika mchakato wa kumuuza straika wa kikosi hicho, Steven Mukwala na imefikia makubaliano na Singida kumchukua mshambuliaji huyo aliyemaliza na mabaon13 kupitia mechi 14 za Ligi Kuu.

“Ni kweli mchezaji amesaini mkataba wa kuitumikia Simba msimu ujao, haikuwa rahisi lakini kutokana na mahitaji muhimu ya kocha uongozi umefanikisha dili hilo,” amesema mtoa taarifa huyo kutoka Simba.

Mwanaspoti limefanya jituhada za kutafuta usahihi wa taarifa hizo kutoka Singida Black Stars ambapo pia wamekiri kuwepo kwa mazungumzo baada ya Simba kutuma ofa ya kuhitaji huduma ya mchezaji huyo.

“Sio mara ya kwanza Simba kuonyesha nia ya kumhitaji Sowah,  naweza kukiri wamerudi kwa mara ya pili baada ya awali kufanya hivyo na kushindwana. Sitakuwa sahihi kukuthibitishia hili kwa sasa sina taarifa hiyo,” amesema mtoa taarifa huyo na kuongeza;

“Sowah ni mchezaji mzuri hakuna timu isiyomhitaji kutokana na ubora alionao nafikiri kiwango alichokionyesha kila kocha anatamani kuwa na mchezaji kama yeye.”

Sowah amejiunga na Singida Black Stars dirisha dogo la usajili akitokea Aln Nasr Beghanzi ya Libya, pia amewahi kuitumikia Medeama ya Ghana.