ABC iliona joto la kufungwa katika Ligi ya kikapu Dar es Salaam (BDL), baada ya kuchapwa na Stein Warriors kwa pointi 74-50.
Mchezo huo uliokuwa mkali na kusisimua, ulipigwa Jumapili usiku katika Uwanja wa Donbosco, Upanga.
ABC iliyokuwa haijapoteza mchezo wowote kwa michezo saba iliyocheza, katika mchezo wa nane ulikuwa ndiyo mchezo wake wa kwanza kupoteza.
Stein Warriors inayoongoza kuwa na wapenzi wengi, kulinganisha na timu zote zinazoshiriki, katika ligi hiyo imeonekana ndiyo tishio kutokana na kiwango kikubwa inachokionyesha.
Katika mchezo huo, Jonas Mushi, Tyrone Edward, na Brin Mramba walikuwa kivutio katika mchezo huo na upande wa ABC alikuwa Elias Nshishi na Alinani Msongole.
Kocha mkuu wa Stein Warriors Karabani Karabani, alisema baada ya kupanda daraja mwaka huu, mipango waliyoiweka ni kufanya vizuri katika Ligi ya BDL na baadaye kucheza mashindano ya ubingwa ya Afrika (BAL).