TIMU ya Independiente Santa Fe, imeonyesha nia ya kumuhitaji mshambuliaji wa Azam FC raia wa Colombia, Jhonier Blanco kwa ajili ya kukichezea kikosi hicho, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa baina ya klabu hizo mbili.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zimeeleza Independiente Santa iliyoanzishwa Februari 28, 1941, Bogota Colombia, ikiwa inashiriki Ligi ya Categoria Primera A, imejipanga kumrudisha mchezaji huyo nyumbani na mazungumzo yanaendelea.
Blanco alijiunga na Azam Julai 1, 2024, akitokea Aguilas Doradas ya mji wa Rionegro, inayoshiriki Ligi Kuu ya Colombia, ambapo alisaini mkataba wa miaka minne kukichezea kikosi hicho, huku akiwa amekitumikia msimu mmoja tu wa 2024-2025.
Chanzo kutoka Azam kimeliambia Mwanaspoti ikiwa klabu yoyote itakayomuhitaji mchezaji huyo na kufikia kiasi cha fedha ambacho wanakihitaji watakuwa tayari kumuuza, japo hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa juu ya uhamisho wake.
“Huu ni muda wa usajili na ni wakati wa kuzungumzwa chochote na hatuwezi kuzuia, kikubwa hakuna ofa yoyote iliyoletwa mezani kwetu, ingawa kama itakuwepo na kukubaliana nayo basi sisi tutafanya biashara ya kumuuza,” kilisema chanzo hicho.
Tangu ajiunge na Azam, Blanco amekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka, ambapo msimu wa 2024-2025, katika Ligi Kuu Bara aliifungia timu hiyo mabao matatu, licha ya kutabiriwa makubwa na mashabiki wa kikosi hicho tangu alipowasili.
Blanco aliyezaliwa Oktoba 18, 2000, alianzia soka lake kwenye akademi ya Club Deportivo Estudiantil kabla ya kujiunga na timu ya Ligi Kuu ya Aguilas Doradas ambayo ilimtoa kwa mkopo kuichezea Fortaleza CEIF ya Ligi Daraja la kwanza Colombia.
Akiwa na Fortaleza, nyota huyo alikuwa mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza Colombia (Categoria Primera B), baada ya kufunga mabao 13, msimu wa 2022-2023 na kukiwezesha kikosi hicho kupanda daraja, huku kikitwaa pia ubingwa msimu huo.