Dar es Salaam. Mipaka, rasilimali, makabila, dini, siasa na kuwa na vijana wengi wasomi bila ajira, vimetajwa kuwa vyanzo vya migogoro inayotokea katika nchi za ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania, zipo baadhi ya nchi za ukanda huo zinakumbwa na vyanzo zaidi ya kimoja kwa pamoja, na hivyo hali ya migogoro kuwa kubwa zaidi.
Kutokana na hayo, Tanzania chini ya uenyekiti wake wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, imekuja na mfumo maalumu wa kubaini viashiria vya migogoro mapema kabla haujatokea ndani ya ukanda huo.
Hayo yanakuja katika kipindi ambacho baadhi ya mataifa ya ukanda huo yanakabiliwa na migogoro, ikiwemo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).
Kauli hiyo imetolewa leo, Jumatano Julai 23, 2025 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alipozungumza na wanahabari kuhusu mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri ya Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika nchi wanachama wa SADC.
Amesema mara nyingi vyanzo vya migogoro katika ukanda huo ni mipaka, na ukizingatia haikuchorwa na Waafrika bali wakoloni, hali inakuwa mbaya.
“Unakuta ndugu wa familia moja, lakini huyu amezaliwa nchi hii na yule nchi nyingine, kwa sababu ya mipaka wanatenganishwa uraia na kuanza migogoro isiyo ya lazima,” amesema.
Makabila nayo, amesema, ni chanzo kingine cha migogoro, ingawa lililopo nchi moja wakati mwingine linafanana na nchi nyingine, tofauti inabaki kwenye majina.
“Dini na siasa ni vyanzo vingine, lakini hata rasilimali ndicho chanzo kilichojitokeza kwa siku za karibuni,” ameeleza.
Chanzo kingine, amesema, ni nchi zenye vijana wengi waliosoma lakini hawana ajira, ndiyo maana Tanzania imeanzisha programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) kutengeneza fursa za ajira kwa vijana.
Balozi Kombo amesema chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, umeanzishwa mfumo wa kubaini viashiria vya mgogoro kabla haujatokea ili udhibitiwe.
Amesema hilo ni moja kati ya mengi ambayo Tanzania inajivunia katika kipindi cha mwaka mmoja wa uenyekiti wake wa asasi hiyo, unaokwenda kuisha Agosti na kukabidhi kwa Malawi kwa mujibu wa kanuni.
Katika uenyekiti wa Tanzania, amesema, amani, usalama na siasa katika ukanda wa SADC zimeendelezwa.
“Oktoba na Novemba Tanzania iliongoza ujumbe wa uangalizi wa uchaguzi Msumbiji, Botswana, Mauritius na Namibia. Yote hayo yanalenga kuimarisha demokrasia miongoni mwa nchi wanachama,” amesema.
Katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, amesema, Tanzania iliratibu mikutano mitano ya wakuu wa nchi kati ya Novemba 2024 hadi Machi 2025.
“Tanzania ilikuwa mwenyeji na mwenyekiti wa mkutano wa maofisa waandamizi wa diplomasia na ulipitia maendeleo ya mfumo wa kuheshimu waasisi wa SADC, ikiwemo kuangalia ujenzi wa sanamu tisa za waasisi hao,” ameeleza Balozi Kombo.
Waziri huyo amesema ndani ya kipindi hicho Tanzania ilichangia wanajeshi na vifaa mbalimbali DRC kupitia operesheni ya kulinda amani ya SAMISADC.
Sambamba na hilo, amesema, hata hatua ya kurejesha vifaa na wanajeshi wake kwa amani imefanyika na sasa imekamilika bila kuleta athari yoyote.
Ni katika kipindi hicho, amesema, ndipo historia na sifa ya pekee ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC zilifanya mkutano nchini, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa jumuiya hizo.
Kuhusu mkutano wa mawaziri, amesema utawahusisha mawaziri na maofisa waandamizi wanaoshughulikia mambo ya nje, ulinzi na usalama kutoka nchi zote wanachama wa SADC.
Mkutano huo, amesema, utafanyika kuanzia Julai 24 hadi 25, mwaka huu na utapitia masuala muhimu ya usalama, tathmini ya mafanikio ya pamoja, na kupanga mikakati ya kushughulikia changamoto za kisiasa katika nchi wanachama.
“Tutajadili kuongezeka kwa migogoro na kupendekeza mbinu za kutatua migogoro na vipimo vya viashiria vya migogoro,” ameeleza.
Mbali na kuimarisha ushirikiano wa kikanda, amesema, hiyo ni fursa ya kimkakati kwa Tanzania kuonyesha urithi wake wa kitamaduni, huduma ya ukarimu na utalii, na tayari wageni zaidi ya 400 wapo nchini kuhudhuria.
Akizungumzia hilo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Lazaro Swai amesema migogoro katika ukanda wa SADC itatatuliwa kwa kuchimbua vyake vyake.
Ameeleza kuwa hatua ya kuwa na mfumo wa kubaini viashiria vya mgogoro itasaidia kudhibiti mapema kabla haijatokea, na hivyo kunusuru athari tarajiwa.
“Hii inaweza kuwa hatua muhimu kwa SADC kuwa na mfumo huu, lakini tuzingatie kuchimbua visababishi vya migogoro ili kufanikiwa kudhibiti mapema,” amesema.