Lindi. Maofisa tarafa pamoja na watendaji wa kata wa Mkoa wa Lindi wametakiwa kuonyesha nidhamu, maadili mema, na weledi wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao.
Pia, wametakiwa kuhifadhi kwa makini siri za Serikali, za wananchi ili kudumisha uaminifu na ushirikiano mzuri baina yao na jamii.
Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Telack akizungumza na watumishi kutoka mikoa minne ya Lindi ,Mtwara ,Pwani na Dar es Salaam.Picha na Bahati Mwatesa
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, wakati wa kufunga mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo watumishi hao, yaliyofanyika leo Jumatano, Julai 2025, yaliyoandaliwa na Tume ya Utumishi wa Umma.
“Watumishi wote wanatakiwa kwenda na msimamo thabiti wa kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao, kwa kuzingatia nidhamu, weledi na uaminifu. Kutunza siri za Serikali pamoja na siri za wananchi ni wajibu mkubwa unaoiheshimisha Serikali na umma kwa ujumla,” amesema.
Pia amewataka kuhakikisha mafunzo waliyopewa yanakuwa chachu ya maendeleo endelevu, na kuwahimiza wasikubali kuwa vikwazo vinavyorudisha nyuma maendeleo katika maeneo yao.
“Huu ni wakati wa kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya. Tunahitaji watumishi wa umma wenye misimamo mikali ya kuleta maendeleo na si vinginevyo,” amesisitiza Telack.
Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo yamejumuisha mada mbalimbali ikiwemo uadilifu kazini, usimamizi wa miradi, maadili ya utumishi wa umma, na umuhimu wa usiri wa Serikali na wananchi, ili kuhakikisha huduma bora na yenye tija kwa wananchi inatolewa.

Pia, amewataka kwenda kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao na wasiende kujiingiza kwenye mianya ya upotevu wa mapato.
Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Sijali Korojelo, amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha watumishi wapya wa umma kwa kuwapatia ujuzi na maarifa muhimu.
Mpoki Mwansisya mtendaji kata ya Nanyamba mkoani Mtwara amesema kuwa mafunzo waliyoyapata watakwenda kuyafanyia kazi kwa ufanisi kwa kufuata miongozo na maadili ya utumishi wa umma.
Naye Sofia Jacob kutoka Mkoa wa Mtwara ameishukuru Tume ya Utumishi wa Umma kwa kuandaa mafunzo hayo kwani wamepata mwanga mkubwa wa kuweza kufanya kazi kwa bidii na juhudi.