Wajibu wa Polisi, vyombo vya habari kudumisha amani Uchaguzi Mkuu

Unguja. Wakati taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, waandishi wa habari kisiwani hapa wametakiwa kuzitumia kalamu zao katika kulijenga taifa lenye amani na utulivu.

Hayo yamebainishwa Julai 23, 2025 na Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, CP Kombo Khamis Kombo wakati akifungua kongamano la kuimarisha amani kupitia hoja na mijadala ya maendeleo baina ya Jeshi hilo na vyombo vya habari lililofanyika Ziwani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Kamishna Kombo amewakumbusha waandishi kuwa kalamu zao ndio hazina ya kujenga amani kwani zina nguvu kubwa ya kuleta umoja na mshikamano au kuleta mizozo katika jamii.

“Waandishi wa Habari muna wajibu wa kuzitumia kalamu zenu vizuri kuhakikisha nchi inabaki katika hali ya amani, umoja na mshikamano kabla, baada na wakati wa uchaguzi kwani kalamu hizo endapo zikitumika vibaya zinaweza kusababisha vurugu,” amesema CP Kombo.

Amesema, licha ya uchaguzi kuwa sehemu ya mchakato wa kidemokrasia, lakini kipindi hicho huibua hisia mbaya miongoni mwa wananchi, hivyo inapaswa kuweka mkazo kwenye kuhubiri amani.

Amefahamisha kuwa, Jeshi la Polisi lina dhamira ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira salama, jambo hilo haliwezi kufanikiwa bila ya ushirikiano wa Jeshi hilo na vyombo vya habari.

Kamishna Kombo amesema hiyo ndio sababu mojawapo ya kuaandaa kongamano hilo ambalo limelenga kujadili na kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati Jeshi na Vyombo vya Habari ili kudumisha amani na utulivu wakati wote.

Ameeleza kuwa, vyombo habari vina nguvu ya kuimarisha au kuvuruga amani kulingana na namna kinavyowasilisha taarifa zake kwa jamii.

“Tunatambua kuwa kalamu ya mwandishi inaweza kuwa chombo cha kuleta utulivu au taharuki, ndio maana tunasisitiza utoaji wa taarifa sahihi, zisizo na upendeleo ili kuepusha migogoro,” alisema CP Kombo.

Naye Mkuu wa Utawala Kamisheni ya Polisi Zanzibar, DCP, Simon Chillery amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu kwa maofisa wa usalama na wanahabari kuimarisha uelewa wa pamoja kuhusu kuilinda amani ya nchi.

“Tuna wajibu wa kuwafikia wananchi na kuwaeleza kwa uwazi umuhimu wa kudumisha amani, pamoja na haki zao za kikatiba wakati wa uchaguzi,” amesema Chillery.

Ameongezea kwamba, kila raia ana haki ya kupata uelewa wa kutosha kuhusu wajibu wao kwa lengo la kushiriki katika uchaguzi kwa njia ya kidemokrasia na utulivu.

Awali, Mratibu wa Kongamano hilo, Ramadhan Himid amesema wajibu wa vyombo vya habari kuelimisha jamii kuhakikisha wanalinda amani wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi ili nchi iendelee kupiga hatua za kimaendeleo.

Ametumia fursa hiyo, kuiasa jamii kujizuia na fitna, vurugu, fujo na chokochoko ili nchi iendelee kukua kiuchumi kwani vitu hivyo haviangalii vya kumuathiri wakati vinapotokea.