WANANCHI wa Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro wameanza jitihada za kurejesha uoto wa asili katika Milima ya Nguru iliyoharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji Miti na kilimo kwa kupanda Miti ya asili kuzunguka safu za milima hiyo.
Sambamba na hatua hiyo, wananchi hao sasa wameanza kuona fursa za kiuchumi kupitia kilimo hicho cha miti ya asili kinachotekelezwa kwa ushirikiano kati ya taasisi ya PAMS Foundation na Serikali kupitia vijiji husika kwa kupata Ajira na kupimiwa mashamba yao.
Mradi huo, ambao tayari umewezesha upandaji wa zaidi ya miche 425,000 ya miti ya asili, umejikita katika vijiji vitano vya awali, huku wananchi wakishirikishwa moja kwa moja kupitia mikataba ya hiyari ya kutenga mashamba kwa ajili ya miti.
Wananchi wanaolima miti hiyo wanalipwa fidia kila mwaka ya maeneo yao huku matarajio makubwa yakiwa kwenye faida ya mauzo ya hewa ukaa baada ya miaka mitano.
“Huu si mradi tu wa mazingira, ni mkombozi wa kiuchumi kwa wananchi wa vijijini,” alisema Maximilian Jenes, Meneja wa Mradi kutoka PAMS Foundation.
Aliongeza kuwa kila mkulima anayeshiriki hupimiwa shamba lake,kijiji hupangiwa matumizi bora ya Ardhi, na hatimaye mmiliki wa shamba hulipwa kwa ardhi yake kutumika kwa kilimo cha miti.
Mbali na faida za kifedha, mradi huo umefungua milango ya ajira kwa wakazi wa vijiji kwa kazi za kulima, kupanda, kupalilia na kuhudumia vitalu vya miche pamoja na ukusanyaji wa mbegu za asili.
Rosemary Mgumya, msimamizi wa kitalu cha miti katika kijiji cha Pemba, anasema “wananchi ndiyo nguzo ya mradi huu.
Tunawahamasisha wenye moyo wa kazi, tunaunda vikundi vyao, na tunahakikisha mashamba yanakuwa safi na miti inakua kwa ubora unaotakiwa.”
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, alitembelea kijiji cha Pemba Katika moja wapo ya maeneo ya mradi na kusisitiza kuwa “jamii inatakiwa ibebe dhamana ya mazingira,” akionya kuwa bila hatua za haraka, rasilimali za asili zinaweza kutoweka.
Mradi huo unalenga kufikia vijiji 25 katika Wilaya ya Mvomero, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vitalu vyenye aina 120 za miti ili kulinda bayoanuwai na vyanzo vya maji vya milima ya Nguru.