Wananchi wataka wizi wa karafuu udhibitiwe, Serikali yatoa kauli

Pemba. Wizi wa karafuu umezua hofu kubwa kwa wananchi wa Shehia ya Mgelema, Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Wameiomba Serikali kuanzisha operesheni maalumu za kuwakamata wahalifu wanaojihusisha na wizi wa zao hilo, ambao umesababisha umaskini mkubwa miongoni mwa wakulima.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na  Mwananchi katika Kijiji cha Mgelema wilayani humo, Julai 23, 2025 wamesema wizi wa zao hilo limekuwa ni changamoto kubwa kwani hushambuliwa na watu wasiofahamika kwa kuziiba zikiwa bado hazijafikia wakati wa kuvunwa, jambo linalowarudisha nyuma katika kujiimarisha kiuchumi.

Bimkubwa Omar Khatib mkazi wa Mgelema amesema kamati ya ulinzi inapaswa kufanya msako kwenye kijiji chao kuwasaka wahalifu wa zao hilo, waweze kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.

“Wakulima wanaomiliki mashamba ya mikarafuu wanakuwa hawana raha wakati mashamba yao yanapozaa maana wezi wanakuwa ni wengi, hivyo kamati ya ulinzi inahitaji kusimamia zao hili kikamilifu,” amesema.

Amesema wengine wamekuwa wakiuhujumu miti hiyo kwa kukata mkaa na kuni hali inayowakwaza katika kuliendeleza zao hilo.

‘’Tunaiomba kamati ya ulinzi na usalama kufanya operesheni maalumu katika kijiji chetu kwa lengo la kuwasaka wizi wanaolihujumu zao letu, karafuu zinaibiwa wakati zikiwa hazijaanza kuvunwa,‘’ amesema Bimkubwa.

Issa Hamdan Maalim amesema changamoto nyingine ni upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wa karafuu ili kuendeleza zao hilo muhimu kwa Taifa.

Maalim amesema wakulima wengi wamekamilisha taratibu za kuomba mikopo hiyo na wameiomba Serikali kuhakikisha inapatikana kwa wakati, ili waweze kuendeleza na kukuza kilimo cha karafuu katika visiwa vya Pemba.

Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Mgeni Khatib Yahya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo, amewatoa hofu wananchi hao kuwa Serikali italisimamia zao hilo na kuwachukulia hatua za kisheria wanaojihusisha na wizi huku akipiga marufuku wanunuzi wasio halali mitaani.

Amesema kamati ya ulinzi na usalama itafanya msako katika shehia tofauti zenye zao la karafuu Kisiwani hapa, ili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria na kuwaomba wananchi kutoa mashirikiano na kuacha muhali katika kufanikisha jambo hilo.

‘’Niwatoe hofu wananchi wa Mgelema kamati ya ulinzi ya usalama itasimamia kikamilifu zao hilo, niwaombe wakulima mtoe ushirikiano na muache muhali pindi tutakapomkamata anayehusika,” amesema Mgeni.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mikopo kwa wakulima wa zao hilo, Mkurugenzi  Mtendaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), Sudi Said Ali amesema wapo katika mchakato wa kulifanyia kazi na muda mfupi watatoa mikopo hiyo.

Ameeleza wapo baadhi ya wakulima walishaleta maombi wanayashughulikia kwani tayari walishafanya mazungumzo na taasisi inayohusika na mikopo (ZEEA) na muda mfupi watatoa, huku akiwaomba wakulima ambao hawajafanya maombi waharakishe ili wajumuishwe na wenzao.