Wito huo umetolewa na Mratibu wa Mkoa wa Mafunzo Ndg. Tumaini Ng’unga kwa Niaba ya Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe.Magdalena Rwebangira wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa Watendaji ngazi ya Jimbo ambapo amewasisitiza kuwa endapo watakiuka viapo hivyo watakuwa wamevunja sheria na watawajibika kwa kutenda kosa hilo.
Aidha Ndg. Ng’unga amewataka Watendaji hao kuhakikisha wanajiridhisha na taarifa kabla ya kuzitoa kwenye vyombo vya Habari na kuipima taarifa wanayotaka kuitoa ili kuepuka kuleta taharuki katika jamii.
“Washiriki wa mafunzo katika utekelezaji wa majukumu yenu mnapaswa kutoa taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya Habari ili kuwajulisha wananchi na wadau mambo mbalimbali ya uchaguzi, Sasa nitumie fursa hii kuwasihi kwamba iwapo kutakuwa na uhitaji wa kutoa taarifa jiridhisheni kwanza na ikiwezekana washirikisheni wenzenu…kabla ya kutoa taarifa…ili kuepuka kuleta taharuki” Ameeleza Ndg. Ng’unga
Mafunzo haya yenye lengo la kuwajengea uwezo watendaji wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo kutoka mikoa ya Rukwa na Katavi yamemalizika leo tarehe 23 Julai, 2025.