Dar es Salaam. Wakati Pato la Taifa (GDP) likikadiriwa kukua kufikia asilimia 6.1 mwaka 2025, upanuzi katika sekta za Tehama, nishati, madini, fursa kwa uvumbuzi wa kifedha na huduma jumuishi za kibenki ni miongoni mwa sababu zinazofanya soko la kifedha Tanzania kutolewa macho na wawekezaji.
Imeelezwa soko la Tanzania lina uwezo mkubwa katika mageuzi ya kiuchumi kupitia uwekezaji wa kifedha ikiwemo benki.
Hayo yamejiri katika ziara ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Absa Group, Kenny Fihla, nchini Tanzania wiki hii kama sehemu ya ziara ya ukanda wa Afrika Mashariki inayolenga kuimarisha dhamira ya kukuza uchumi wa kikanda, ujumuishaji wa kifedha endelevu, na kuimarisha huduma kwa wateja.
Ziara hiyo inaonesha utambuzi wa Absa kwa Tanzania kama soko muhimu katika Afrika Mashariki ambapo uongozi wa benki umetumia fursa ya ziara hiyo kuchunguza namna unavyoweza kuendelea kusaidia mageuzi ya kiuchumi, hususan katika maeneo ya teknolojia ya kifedha (fintech), fedha za biashara na uwezeshaji wa vijana.
“Tanzania ni soko lenye uwezo mkubwa, na uwepo wetu hapa haupaswi kuishia tu kwenye utoaji wa huduma za kifedha, bali uwe ushirikiano, malengo na maendeleo. Lengo letu ni kuwa na ari ya kumjali mteja, kwa kusikiliza zaidi, kuchukua hatua haraka na kutoa suluhisho zinazohusiana moja kwa moja na maisha na biashara za Watanzania, tuko hapa kujenga uhusiano wa kudumu na kukua pamoja na jamii tunazozihudumia,” amesema.
Ziara hii ni sehemu ya kwanza ya kampeni pana ya Absa ya kutembelea nchi mbalimbali chini ya Absa Regional Operations (ARO), inayojumuisha soko lingine muhimu.
Pia, inaendana na mkakati wa Absa barani Afrika wa kuimarisha uwepo wake katika nchi zenye ukuaji wa haraka na kusaidia ujumuishaji wa kikanda kupitia ubunifu wa kidijitali, uendelezaji wa biashara ndogo ndogo, na malengo ya fedha endelevu.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Obedi Laiser, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa nchini, amesema: “Ziara hiyo inathibitisha umuhimu wa kimkakati wa soko la Tanzania katika mtandao wa Absa barani Afrika na inaonesha kuendelea kwa imani katika safari yetu ya ukuaji,” amesema.
Theobald Sabi, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, benki ambayo Absa inamiliki hisa nyingi, amesema: “Kama mbia wetu mkuu, Absa inaendelea kuwa nguzo muhimu katika safari yetu ya ukuaji. Ziara hii ya viongozi wetu wakuu inathibitisha nafasi muhimu ya Tanzania katika mtandao wa Absa barani Afrika na inaonesha nguvu ya dhamira yetu ya pamoja.