Dodoma. Serikali imehimizwa kutumia wazee wa mila katika juhudi za kulinda mazingira, kwani bila ushirikiano wao hali inaweza kuwa mbaya zaidi na migogoro kuongezeka.
Ushauri huo umetolewa leo Jumatano Julai 23, 2024, na Mzee wa mila (Laigwanani) Lameck Kampu kutoka jamii ya wafugaji Kata ya Patimbo, Wilaya ya Kiteto.
Ameeleza kuwa migogoro mingi hutokea kila kukicha kutokana na mgongano wa maeneo yenye rutuba, hasa baada ya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji holela wa miti katika baadhi ya maeneo.
Mzee Lameck ametoa ushauri huo wakati wa kongamano la siku moja la watetezi wa mazingira lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), likiwa na wadau mbalimbali wakiwemo wasomi wa vyuo vikuu na wanamtandao wa mazingira.
Amebainisha kuwa chanzo kikuu cha migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kiteto ni uharibifu wa mazingira, unaosababisha kila kundi kutafuta maeneo yenye rutuba, wakulima kwa ajili ya kilimo na wafugaji kwa ajili ya malisho.
“Wanaleta viongozi kutoka maeneo tofauti wanakuja na kuanza kutoza faini na kukamata watu, kumbe jamii ilipaswa kupewa elimu kwanza kabla ya kufikia huko, tambueni mtu wa eneo husika anaweza kutoa elimu nzuri zaidi msomi na kuna sheria zetu za jinsi ya kubanana na watu hao kuliko mgeni ingawa hatuwakatai wataalamu,” amesema Kampu.
Laigwanani huyo amebainisha kuwa viongozi wa mila wana sheria zao na wanaweza kumtambua kwa haraka mtu aliyezivunja kuliko kama ilivyo sasa ambapo wenyeji wakibaini mwenzao kakosea hupanga mkakati wa kumlinda.
Amesema wakulima wamekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira kwa kufungua mashamba mapya.
Hata hivyo, ameonya kwamba wafugaji nao wanachangia uharibifu kwa kuingilia mashamba, kuchunguza mifugo, na kutafuta maji baada ya mabwawa ya asili kukauka kutokana na ukataji miti na matumizi mabaya ya ardhi katika kilimo.
Spora Samuel kutoka jamii ya Barbaig wilayani Hanang amesema katika maeneo yao, mtu pekee anayesikilizwa ni mzee wa mila ambaye ana uwezo wa kuwasiliana na jamii kwa lugha ya mawanda pana na kueleweka vizuri.
Spora amebainisha kuwa ukosefu wa elimu ni changamoto katika mawasiliano, na mara nyingine wataalamu hawajui asili ya maeneo hayo, jambo linalosababisha hata miti inayopandwa kuishi kwa muda mfupi tu kwa sababu hawajui msimu na aina sahihi ya miti inayopaswa kupandwa.
Mratibu wa mradi wa Mazingira kutoka LHRC, Fundikila Wazambi amesema katika tafiti walizofanya hivi karibuni Wilaya za Kiteto hali ya mazingira ni mbaya, lakini wameanza kutoa ushauri wa kuwashirikisha wenyeji zaidi katika utunzaji wa mazingira.
Fundikila amesema lengo la kuwafikisha pamoja watetezi wa mazingira ni kuandaa andiko la pamoja litakalowasilishwa kwa mamlaka husika, likipendekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa ajili ya kulinda mazingira.
Hata hivyo, amekiri kuwa wataendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wananchi na wadau wengine ili kuhakikisha kila mtu atambue jukumu lake la kuhifadhi na kulinda mazingira.