………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea Chuo Kikuu cha Kilimo cha Belarus (Belarusian State Agrarian Technical University – BSATU) na kufanya mazungumzo na viongozi wa chuo hicho wakiongozwa na Mkuu wa Chuo, Bw. Romaniuk Nikolai.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo (Jumatano, Julai 23, 2025) kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo hicho jijini Minsk ambapo masuala ya ushirikiano baina ya vyuo vikuu vya Tanzania vikiwemo vya Sokoine na DIT yalijadiliwa.
Waziri Mkuu aliwaeleza viongozi wa chuo kikuu hicho jinsi Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilivyoboresha sera ya elimu ambayo inataka elimu ya amali na stadi za ufundi ziwe sehemu muhimu katika mitaala ya mafunzo yanayotolewa nchini kote.
Aliwaeleza viongozi hao juu ya hati ya makubaliano kwenye sekta ya elimu iliyosainiwa jana mbele ya Waziri Mkuu wa Belarus na kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuangalia namna ya kuandaa ziara za mafunzo, kubadilishana wanafunzi na wahadhiri ili kujengeana uwezo kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha BSATU, Bw. Romaniuk Nikolai alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba chuo hicho kipo tayari kuanza majadiliano na viongozi kutoka Wizara ya Elimu ambao wamefuatana na Mheshimiwa Waziri Mkuu ili waone ni kwa namna gani wanaweza kuanza kutekeleza mambo yaliyojadiliwa.
Alimweleza Waziri Mkuu kwamba Chuo Kikuu hicho ambacho kilianzishwa mwaka 1954, kinaongoza nchini humo kwa kutoa mafunzo kwenye fani za uhandisi, uchumi na utawala na kinashirikiana na taasisi na mashirika rafiki 39 (affiliate organisations) yanayojihusisha na masuala ya kilimo na uundaji wa mitambo ya kilimo na zana za kisasa.
Alisema wanalenga zaidi fani za kitaalamu kwenye ufugaji wa wanyama na mitambo ya kilimo (animal husbandry and agricultural mechanisation) ambapo asilimia 70 ya mafunzo yanayotolewa chuoni hapo, hufanyika kwa vitendo (practicals) na kisha mwanafunzi anapewa wiki 28 za kwenda nje ya chuo kufanya mafunzo kwa vitendo (internship).
Mapema leo asubuhi, Waziri Mkuu alikutana na Wawakilishi wa Muungano wa Kampuni za Belarus zinazofanya biashara na mataifa ya Afrika (AFTRADE) kwenye ukumbi wa mikutano wa hoteli ya President.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Bw. Shariff Ali Sharriff, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu Katibu Mkuu Kilimo, Dkt. Stephen Nindi na Balozi wa Tanzania nchini Urusi na Belarus, Balozi Fredrick Kibuta.