Yanga yamuongeza Casemiro kikosini | Mwanaspoti

MABINGWA wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC wamekamilisha usajili wa kiungo mkabaji, Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’ kwa mkataba wa miaka mitatu.

Yanga inaendelea kusuka kikosi kwa ajili ya msimu ujao 2025-2026, kwa nia ya kuhakikisha inaendelea pale ilipoishia msimu uliopita 2024-2025 ilipotwaa mataji matano ikiwamo kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).

Mwanaspoti lilianza kuripoti taarifa ya usajili wa kiungo huyo ambaye leo Julai 23, 2025 ametambulishwa rasmi na Yanga akiwa ni mchezaji wa tatu baada ya kuanza na kiungo mkabaji Moussa Balla Conte kutoka CS Sfaxien na winga Offen Chikola aliyetokea Tabora United.

Katika kuhakikisha kila kitu kinaendelea kuwa sawa, mabosi wa Yanga wameamua kuvuka maji ya Bahari ya Hindi na kwenda visiwani Zanzibar kuinasa saini ya kiungo huyo aliyetokea Mlandege.

Casemiro (20) ni miongoni mwa viungo bora waliofanya vizuri katika Ligi Kuu ya Zanzibar msimu uliopita 2024-2025 akicheza mechi zote 30 na kuisaidia Mlandege kutwaa taji la ligi.