Rungwe. Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemwagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa kimkakati wa chanzo cha Mto Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya kuongeza kasi ulazaji mabomba ya kusafirisha maji kwa lengo la kutimiza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan kumtua mama ndoo kichwani.
Mbali na kutoa agizo hilo alilolitoa jana Julai 23, 2025, ameweka banana sababu za ujio wa mradi huo mkubwa wa kimkakati ni ombi la Spika wa Bunge la Dk Tulia Ackson.
Ameeleza kuwa awali baada ya kupokea ombi hilo aliwasilisha kwa Rais Samia ambaye alibariki kwa kuelekeza Serikali kutoa zaidi ya Sh22 bilioni kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake.
“Nipongeze Mkuu wa Mkoa Mkoa (RC), Beno Malisa, Mamlaka ya Maji, Mwenyekiti wa Bodi ya Maji kwa usimamizi na mzuri wa mradi huu mkubwa ambao utakwenda kutatua hadha kwa wanambeya na maeneo ya jirani,” amesema Aweso.
Amesema katika ziara yake kwenye mradi huo ameona kazi kubwa imefanyika kwenye chanzo kwani mwenye macho haambiwi tazama mmeupiga mwingi, lakini tumebaini changamoto juu ya ulazaji wa bomba hapo panahitaji kuongeza nguvu katika utendaji.
“Katika hilo Katibu Mkuu Wizara ya Maji (Mhandisi Mwajuma Waziri), nikutake kuona namna ya kupata kiwanda kinachozalisha mabomba yanayotumika katika mradi huu wenye kulaza mabomba urefu wa kilometa 36 kuna namna waingie mkataba na mkandarasi ili kuzalisha mabomba yatakayo wezesha kukamilisha mradi huu,” amesema.

Amesema endapo watachukua hatua hiyo hakutakuwa na sababu ya kukwama kwa mradi, lakini suala lingine ni nguvu kazi zinahitajika kama wizara tutakaa na mkandarasi katika eneo la kutibu maji la New Forest ili kuhainisha changamoto zilizopo na kuzitatua.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso, amesema amelisikia kwa Mkuu wa Mkoa (RC ) Beno Malisa na kwamba ameanza ziara yake hiyo ni maalumu baada ya Rais kuhainisha miradi ya miji 28 ambayo imeanza kutekelezwa nchini.
“Nimeanza ziara kwa ajenda maalumu ni Rais aliainisha miradi ya miji 28, ambayo amepata fedha kufuatia mahusiano yake aliyojenga na Serikali ya India ambayo imetoa Dola milioni 500 kwa ajili ya utekeleza wa mradi hiyo maeneo mbalimbali.
Amesema kupitia fedha hizo Mkoa wa Mbeya eneo la Rujewa Wilaya ya Mbarali, imenufaika na Sh130 bilioni kutekeleza mradi huo ambao watachukua maji kutoka chanzo cha Mto Mbarali ambayo yatahudumia wananchi wa Kata ya Rujewa Wanging’ombe na Makambako Mkoa wa Njombe.
“Mkuu wa Mkoa mradi huo ni mkubwa, lakini nikupe taarifa nimefika nimepata ushirikiano mkubwa kazi imefanyika tumeridhishwa nimeagiza waongeza kasi wafanye usiku na mchana ifikapo Oktoba mwaka huu uwe umekamilika,” amesema.
Katika hatua nyingine, amemuagiza Mkuu wa Mkoa kusimamia na ufuatiliaji utekelezaji wa mradi wa miji 28, wakati mwingine ipo janja janja ukabaini wewe ruka nao sisi tutabariki ili mambo yaende.
Mkuu wa Mkoa (RC), Malisa alisisitiza wizara kuona namna kuwasaidia Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (Ruwasa) kuwawezeshwa kifedha ili kutekeleza miradi kwa wakati.
“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu wa kimkakati wa maji wa chanzo cha Mto Kiwira ambao utakwenda kuwa chachu kwa wananchi ambapo wanadeni la kutiki katika uchaguzi Mkuu Oktoba 2025,” amesema.
Malisa amesema Serikali imefikia dhima nzima ya kutatua changamoto ya maji, lakini nikuombe kwa niaba ya wanaMbeya kuna miradi 15 itaendelea kutekelezwa na Ruwasa tuombe hilo ulichukue ili iweze kuikamilisha kwa wakati,”amesema.
Mkurugenzi mtendaji Mbeya Uwsa, Gilbert Kayange amesema mradi huo ulianza utekelezaji Aprili 2023 na wanatarajia kukamilika Desemba mwaka huu.
Amesema wao ni wasimamizi wa mradi huo ambao unatekelezwa na mkandarasi wa Kampuni ya China Rarway Construction Engineering Group, chini ya Mhandisi mshauri GkW Consult GmbH.
Kayange amesema mradi huo ulikamilika utazalisha maji lita milioni 117 kwa siku lita ambapo kwa sasa wastani wanazalisha lita 76 milioni huku mahitaji yakiwa lita 90 milioni.
Amesema wana imani ukikamilika kwa mradi huo kutawezesha kukidhi mahitaji ya kuwa na lita 190 milioni kwa siku ambayo yataweza kuhudumia maeneo mbalimbali ikiwepo Mji wa Mbalizi na Mkoa wa Mbeya.
Kayange amesema mradi huo ulisainiwa Machi 2023 kwa gharama ya Sh99 bilioni bila ongezeko la kodi, lakini mwaka 2022 Februari walimpata Mhandisi mshauri ambaye alisaini mkataba wa Sh2.2 bilioni na kufanya gharama za mradi kuwa Sh 119 bilioni na kubainisha ujenzi umefikia asilimia 45.
Mkazi wa Kijiji cha Simambwe, Sarah Abraham ameishukuru Serikali kwa kuja na mradi huo wa kimkakati ambao utaleta tija kubwa ya kuondoa hadha ya maji safi na salama.
Amesema mradi huo utaongeza chachu ya wananchi kuzalisha shughuli za kiuchumi na kuepuka kutumia muda mwingi kusaka rasilimali hiyo.