LIGI ya Kikapu Dar es Salaam (BDL) inayoshirikisha timu za wanaume na wanawake, imezidi kushika hisia za wengi huku baadhi ya watu wakifungwa midomo baada ya kuona miamba miwili wa msimu uliopita Dar City na Tausi Royals msimu huu zitachemsha.
Timu hizo zimeendeleza ubabe katika ligi hiyo zikionyesha wazi zilijiandaa kufanya makubwa tofauti na wengi walivyotarajia, huku Tausi ya upande wa wanawake ikiendeleza moto kwa kushinda dhidi ya DB Trancatti na City ikiichapa BD Oratory wikiendi iliyopita, kwenye Uwanja wa Donbosco Upanga, jijini Dar es Salaam.
Tausi ilishinda pointi 78-48 dhidi ya DB Trancatti, huku ikitawala mchezo huo robo zote kwa pointi kuongoza kwa pointi 22-13, 13-11, 24-6 na 19-18, huku Juliana Sambwe wa Tausi akifunga pointi 28, Tukusubira Mwalusamba 19, huku kwa DB Troncatti, Jesca Lenga alifunga 18 na Irene Gerwin 17.
Tausi ilionyesha ubabe huo licha ya kutopata sapoti ya kutoka kwa baadhi ya timu zilizokuwa zikishangilia zilizofanya vizuri, huku lawama zikitupwa kwa waamuzi kwa madai hawakupiga filimbi wakati wachezaji wa DB Trancatti wakifanyiwa madhambi.

Mchezo wa Dar City dhidi ya DB Oratory mabingwa hao wa msimu uliopita waliendeleza ubabe kwa kuichapa wapinzani wao kwa pointi 76-53, ikibebwa zaidi na uwezo wao, huku wengine wakiona inapendelewa.
Katika mchezo huo, lawama hizo zilikuja baada ya kuonekana City imezidiwa kiwango na wapinzani ingawa waliamua kucheza na kufunga wakitumia kufunga katika eneo la mtupo mmoja wa pointi tatu, hali iliyofanya watulie.
Dar City katika mchezo huo iliwachezesha wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao ni Jamel Marbuary wa Marekani, Victor Mwoka (Kenya), Sharom Ikedigwe (Nigeria), Clinton Best, Mhangachi Atibu na Amin Mkosa.
Dar City iliongoza robo zote nne kwa pointi 19-17, 17-6, 17-15 na 23-15, huku nyota wake Ikedigwe akifunga pointi 18 na Mkosa 15, huku kwa upande wa DB Oratory, Hassan Kabanda alifunga pointi 16 na Isaya Wlliamu 14, huku timu hizo zikipongezana baada ya mchezo huo.

Reel Dream kuongeza vifaa vipya
Baada ya ushindi wa pointi 94-30 dhidi ya UDSM Queens, Kiongozi wa Reel Dream ambayo ndiyo mara ya kwanza kushiriki ligi hiyo, Emmanuel Mkono amesema endapo timu yake itatinga robo fainali ya WBDL wataongeza wachezaji wengine.
“Nina imani tutacheza robo fainali na ligi hii kwa sasa tumeizoea, tutatambuana itakapomalizika,” alitamba Mkono.
Katika mchezo huo Reel Dream iliongoza robo zote nne kwa pointi 28-9, 26-4, 17-11 na 23-6, huku Husna Mwengelo akiongoza kwa kufunga pointi 21, na Maryshallet Shibweche 17 na kwa upande wa UDSM Queens Lina Ngombeni alifunga pointi 7 na Najaha Rashidi 6.

JKT yaifanyizia Savio kibabe
Haikuwa rahisi kwa JKT kuifunga timu ngumu ya Savio kwa pointi 65-56 katika mchezo uliopingwa kwenye uwanja huo na kuzidi kuongeza ushindani wa ligi hiyo zikisaka nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali.
Baada ya mchezo huo kumalizika wapenzi waliofurika uwanjani hapo, waliondoka wakiwa wameridhika na kiwango kilichoonyeshwa na timu zote mbili.
Omary Sadiki wa JKT, ndiye aliyepeleka kilio kwa Savio baada ya kufunga pointi 26, huku akifunga eneo moja la mtupo mmoja wa three pointi tisa, akifuatiwa na Baraka Sabibi aliyefunga 20 na upande wa rebound Jimmy Brown alidaka mara 15 na kuzuia ‘blocks’ sita. Kwa upande wa Savio alikuwa Ntibonera Bukengu aliyefunga 26 na Godfrey Swai 12.

Kurasini Divas yageuzwa uchochoro
Wakati baadhi ya timu zikiwa zimecheza michezo 10, imeonyesha Kurasini Divas ndiyo inayongoza kwa kuruhusu kufungwa pointi nyingi, 852, ikifuatiwa na UDSM Queens pointi 810, City Queens (722), Kigamboni Queens (577, Mgulani Stars (543), Reem Dream 522, Polisi Stars (482) na Pazi Queens (453), DB Troncatti 428, Twalipo Queens (340), DB Lioness (333), JKT Stars (302), Vijana Queens (300), Jeshi Stars (282)na Tausi Royals (287).