Chalamila awaomba radhi watumiaji wa mwendokasi

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewaomba radhi wakazi wa Kimara kuhusu adha wanayopitia wanapohitaji kutumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka, ikiwemo kupita dirishani.

Ametoa kauli hiyo huku akiwapa ahadi ya neema siku chache zijazo, wakati ambao mabasi mapya yanatarajiwa kupokelewa.

Haya yanasemwa wakati ambao Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) imeeleza sababu ya magari mengi yaliyoharibika kutotengenezwa kwa wakati, hali inayosababisha magari machache kuwa tegemezi katika utoaji wa huduma.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Julai 24, 2025 jijini humo, wakati mkuu huyo wa mkoa alipofanya ukaguzi wa utoaji huduma wa mabasi hayo katika kituo cha Kimara, ambacho mara zote hulalamikiwa.

Malalamiko hayo yanatokana na watu kutumia muda mrefu kusubiri magari, wakati ambao mengine yanakuwa yamepaki bila sababu zilizowekwa wazi, huku machache yanayokuwapo watu wakiyagombania kwa wengine kupita dirishani, hali inayoleta mminyano.

Chalamila amesema Watanzania kwa sasa wanalia na usafiri huo kwa kuwa kuingia katika basi imekuwa ni vurugu, hali inayoweka ugumu zaidi kwa watu wenye mahitaji maalumu na wajawazito.

“Kwa niaba ya Serikali na wizara zote zinazohusika, kwa ziara ambayo nimefanya na video zinazotembea mitandaoni, niwaombe radhi Watanzania wanaotumia usafiri huu wa mwendokasi. Radhi hii tunaomba kwa sababu tumeona video ambazo baadhi ya watu wanaingia kwenye magari kwa kupitia madirishani,” amesema.

“Pia, baadhi ya video zinaonyesha mvua inanyesha na watu wameshika miamvuli ndani ya magari. Adha hizi zimepokelewa kwa mikono miwili na wizara inayohusika na kuanza kufanyiwa kazi kwa haraka na Mtendaji Mkuu wa DART (Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka),” amesema.

Amesema ili kuboresha huduma, Serikali imealika sekta binafsi zifanye uwekezaji katika utoaji wa huduma, na tayari awamu ya pili ya mradi inayoanzia Gerezani hadi Mbagala amepewa mtoa huduma mzawa, Kampuni ya Mofat, anayetarajiwa kuanza kazi Septemba mwaka huu.

Mtoa huduma huyo anatarajiwa kutoa huduma kwa miaka 12, mabasi 99 ya kwanza yanatarajiwa kufika nchini mwezi ujao, huku mengine yakitarajiwa kuwasili siku 30 baada ya yale ya awali. Hili linafanyika wakati ambao pia njia za mlisho kuelekea vituo vya mradi huo zimepata watoa huduma, ambao wanatarajia kuleta magari 200.

Awamu ya kwanza nayo imepata mtoa huduma anayetarajiwa kuongeza idadi ya mabasi, hali inayotarajiwa kuleta ahueni kwa wakazi wanaohudumiwa na ruti hiyo.

Mtendaji Mkuu wa DART, Dk Athuman Kihamia amewahi kunukuliwa huko nyuma akisema awamu ya kwanza ya njia ya Kimara–Morocco–Kivukoni na Gerezani itaendeshwa na Kampuni ya Emirates National Group (ENG) kwa miaka 12, na wanatarajia kushusha mabasi 177.

Dk Kihamia amekuwa akisisitiza kuwa baada ya wawekezaji hao wazawa kwa njia ya Gerezani–Mbagala na awamu ya kwanza kuanza kazi: “Suala la hali ya usafiri wa kugombania au kusubiria muda mrefu sasa litakuwa historia.”

Hayo yamesemwa wakati ambao mwananchi, Rashid Suleiman, alilalamika kupoteza muda mwingi kituoni hapo huku akishangaa huduma iliyokuwa ikitolewa leo.

“Leo ni ajabu, saa 1 asubuhi kituo kipo tupu, hakuna watu. Magari yanakuja yanaondoka yakiwa hayajajaa. Hali haiko hivi, wameboresha leo wakijua mkuu wa mkoa unakuja. Siku uje bila taarifa, utasukumwa udondoke hapa,” amesema Suleiman, huku akitaka huduma ziboreshwe ili wawe salama.

Sababu za magari kutotengenezwa

Meneja upangaji ratiba na udhibiti kutoka UDART, Daniel Madili amesema magari mengi yaliyoharibika changamoto kubwa ni injini, na bahati mbaya wao kuwa wa kwanza kuanzisha mradi huo umewafanya kukabiliwa na uhaba wa upatikanaji wa vipuri.

“Kwa sasa wasambazaji wa vipuri ni wachache. Mfano, hata wiper ikiharibika lazima tuagize kutoka nje ya nchi, injini na vitu vingine vingi. Tumekuwa na changamoto kuwa wasambazaji waliopo nchini hawana vitu vingi vya kuhudumia haya mabasi,” amesema Madili.

Amesema vifaa hivyo huagizwa kutoka China, hali inayowafanya kutumia ndege au meli hali inayoleta ucheleweshaji na hilo hufanyika pale anapoonekana hakuna msambazaji anayeweza kuleta vitu hivyo.

“Pia kulikuwa na gharama kubwa za uendeshaji, kwani tangu mradi unaanzishwa ilikuwa ikitumika Sh650, tofauti na sasa,” amesema.

Hadi sasa wana magari takribani 60 yanayotoa huduma katika awamu hiyo ya kwanza kati ya yaliyokuwapo wakati mradi unaanza kazi.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amesema kitendo cha wananchi kuchelewa kufika maeneo yao ya kazi kina athari za moja kwa moja katika uchumi.

“Magari mengi yameharibika na mengine yanaharibika barabarani na kusababisha foleni kutokana na kukaa muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo,” amesema huku akitaka waainishe hatua za muda mfupi za kutatua changamoto hiyo.

“Wananchi wako vituoni. Ukimuambia subiri hadi Oktoba au Novemba hawezi kukuelewa kwa sababu anataka kwenda kazini, na wewe kama mwajiri unataka kumuona mfanyakazi wako kazini,” amesema.

“Changamoto iliyopo ni lini au UDART wanajipangaje kutatua changamoto hii kwa muda mfupi, kwa sababu moja ya jukumu walilopewa na Serikali si kulalamika na kutoa ahadi bali kutatua tatizo lililopo,” amesema Msando.

Ili kuondoa muda wa watu kusubiri vituoni, Dk Kihamia amesema watahakikisha watoa huduma wanaopewa kazi hiyo wanasimamia muda katika utoaji huduma.

“Hiki ni moja ya vitu vilivyozingatiwa na vilitumika kama moja ya vigezo vya mtu kushinda zabuni hii. Endapo ikikiukwa, watakuwa wakipigwa faini au kuondolewa kabisa,” amesema Kihamia.