KAMA ulikuwa na fikra kwamba Clatous Chama ndio basi tena katika Ligi Kuu Bara, basi pole kwani kiungo mshambuliaji huyo bado yupo sana na msimu ujao anatarajiwa kukiwasha akiwa na chama jipya la Singida Black Stars.
Nyota huyo raia wa Zambia aliyekuwa akikipiga Yanga iliyomsajili msimu uliopita akitokea Simba na kumaliza na mabao sita na asisti tatu, imedaiwa ameshasaini mkataba wa kuitumikia Singida iliyokata tiketi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2025-2026.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Singida ni kwamba Chama aliyemaliza mkataba na Yanga amepewa mwaka mmoja, ikiwa ni pendekezo la kocha mpya wa kikosi hicho aliyewahi kufanya kazi na Mzambia huyo alipokuwa Jangwani, Miguel Gamondi.
Mkataba huo wa mwaka mmoja wa Chama una kipengele cha kuongezwa na sasa anaungana na nyota wengine aliokuwa nao Yanga, yaani beki wa kushoto, Nickson Kibabage na kiungo Jonas Mkude ambao wameshatangulia mapema Singida BS.
Chanzo cha kuaminika kutoka Singida BS kimelithibitishia Mwanaspoti kuwa, ni kweli Chama na Singida wamemalizana ikiwa ni utekelezaji wa pendekezo ya kocha Gamondi, aliyerejea nchini baada ya kuinoa Yanga kwa misimu miwili na kuiwezesha kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika misimu miwili mfululizo ikiwa ni baada ya kupita miaka 25 tangu iliposhiriki mara ya kwanza 1998.
“Chama atakuwa sehemu ya kikosi chetu msimu ujao tunaamini atatusaidia kwenye mashindano ya ndani na kimataifa kutokana na uzoefu wake lakini pia ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Tuna mashindano mengi msimu ujao lakini pia hatutaki kuwa bora msimu mmoja tunahitaji muendelezo baada ya msimu ulioisha kuishia nafasi ya nne tukipata nafasi ya kushiriki kimataifa tunahitaji kuwa na muendelezo msimu ujao ili kuwa miongoni mwa timu ambazo zitakuwa na uwakirishi mzuri.”
Mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema wanaimani na kiungo huyo na kwa kuwa ni pendekezo la kocha wanaamini atakuwa na mchango mkubwa.
Licha ya Gamondi kupendekeza jina la kiungo huyo ambaye hakuwa chaguo la kwanza kikosi hicho walipokuwa Yanga, lakini kocha huyo aliwahi kutoa ufafanuzi alipoulizwa kwa kuzungumzia ugumu aliokuwa anakutana nao kuwapanga akiwa na namba 10 watatu, Stephane Aziz Ki, Chama na Pacome Zouzoua.
Kocha huyo raia wa Argentina alisema, presha itakuwa kwa wachezaji wenyewe kwani wanatakiwa kupambana kuanzia mazoezini hadi katika mechi ili afanye uamuzi wa kuanza na nani kisha nani atokee benchi.
“Kiukweli najibu tena, sina presha kabisa yaani sina kabisa, kwangu nafurahia tu ujio wa wachezaji bora kama hawa tunategemea watajituma ili Yanga ifanikiwe, labda presha itakuwa kwao itategemea nani anajituma kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi,” alisema Gamondi na kuongeza;
“Siwezi kuchezesha wachezaji wote watatu kwa wakati mmoja ni lazima mmoja ataanzia benchi kusubiri wengine waanze huu ndio mtihani uliopo lakini kuwa na nyota wote bora inaongeza kujiamini kwani ninakuwa na uhakika na nyota walio anzia nje.” Kauli ya Gamondi akiwa Yanga.