Dar es Salaam. Katibu Mkuu Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amesema wanawake wa chama hicho wana uwezo wa kugombea nafasi mbalimbali za udiwani, uwakilishi na ubunge hivyo hawapaswi kulemaa na viti maalumu.
Ikumbukwe nafasi ya viti maalumu ni fursa kwa wanawake katika kushiriki siasa ambapo nafasi hiyo inahusisha uwakilishi katika Bunge la Tanzania, Baraza la wawakilishi Zanzibar na Baraza la Madiwani.
Baada ya mijadala mbalimbali ya kidunia kuhusu usawa wa jinsia na baadaye kupitishwa matamko kadhaa ya kitaifa na kimataifa ya kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo hivyo, mfano tamko la nchi za Jumuiya ya Maendeleo Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuingiza asilimia 30 ya wanawake katika vyombo vya maamuzi au ile kauli mbiu ya awamu ya nne ya 50 kwa 50, umuhimu wa viti maalumu ulizidi kuongezeka nchini.
Hivyo baada ya muda mrefu wa uwakilishi kupitia viti maalumu nafasi ambayo inatokana na chama wanawake wametakiwa kutobweteka na kuwaza kupata nafasi hiyo kupitia chama, bali wakatafute uongozi kupitia mchakato wa kura.

Akizungumza leo Alhamisi, Julai 24, 2025 makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam wakati akipokea mapendekezo ya utaratibu, sifa na vigezo vya viongozi wa viti maalumu kwa wanawake wa chama hicho, Mwalimu amesema wanawake wanaweza kupambana kwenye maboksi ya kura.
Mtendaji huyo mkuu wa chama anayasema hayo wakati ikiwa imesalia miezi miwili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba mwaka huu 2025.
“Unakuta kuna majimbo hayana wagombea wa kutosha lakini kuna maelfu ya wanawake wanakimbilia kwenye viti maalumu kwenye jimbo hilohilo.
“Rai yangu wasikimbilie kwenye viti maalumu, visiwalemaze, wanawake wana uwezo wa kushindana kwenye majimbo wakaomba kura wakapata na wakashinda kwenye kata, jimbo na uwakilishi,” amesema.

Mwalimu amesema chama hicho kimeshaweka kigezo kikuu cha mwanamke kufikiriwa kuwa diwani, mwakilishi au mbunge wa viti maalumu utatokana na mchango wa kura alizozileta kwenye sanduku.
Akipiga hesabu zake amesema haipaswi kutegemea nafasi za viti maalumu bali ikichukuliwa idadi ya wale watakaotoka majimboni, kata ukaongeza na wale watakaotoka kwenye viti maalumu basi watakuwa wengi na itakua na tija zaidi.
Amesema wanawake wanapaswa kuchangamkia fursa zote za viti maalumu na kugombea nafasi hizo kwenye kura.
Akizungumzia mapendekezo aliyopokea amesema kama Katibu Mkuu aliunda kamati ya wanawake kwa ajili ya kutengeneza mapendekezo juu ya utaratibu, sifa na vigezo vya Chaumma katika nafasi za diwani, mjumbe wa baraza la wawakilishi na mbunge wa viti maalumu.
Amesema kamati kuu ndiyo itatoa mapendekezo ya mwisho juu ya mwongozo huo baada ya mapendekezo hayo kupita ngazi nyingine ikiwemo sekretarierti.
Akizungumza na Mwananchi Katibu wa Kamati hiyo ya mapendekezo, Moza Ally amesema suala lililozungumzwa na Katibu Mkuu juu ya wanawake kwenda kugombea ni la msingi na wanawake wa chama hicho wamelipokea.
“Hii itasaidia wanawake kutoegesha kutegemea nafasi za viti maalumu bali wakienda kugombea na endapo hawajafanikiwa ndipo watakuja huku,” amesema.
Akidokeza mapendekezo hayo amesema sifa ya kwanza kubwa ni kuwa mwanachama wa Chaumma, pili kuwa mfanyakazi inayoonekana.
Naye, Ofisa wa chama makao makuu, Rachel Mkadala amesema huwezi kupewa viti maalumu wakati hujaingiza chochote unapaswa angalau kuonesha juhudi.