KATIKA siku za hivi karibuni, picha ya kiungo mkabaji wa Singida Black Stars, Mohammed Damaro, akiwa amevalia jezi ya Yanga, ilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na kuibua mjadala miongoni mwa mashabiki wa soka nchini huku wengi wakihoji uwepo wake ndani ya uzi huo.
Picha hiyo ilizua hisia mbalimbali, wapo waliodhani tayari ametua Jangwani, wengine wakifikiria labda ni aina ya kutangaza nia au kutoa ishara kwa viongozi wa Yanga kuwa yuko tayari kuiwakilisha klabu hiyo.
Sasa Damaro mwenyewe ameamua kuvunja ukimya akiwa mapumzikoni nchini Guinea ambako ndiko ilipo familia yake licha ya kubadili uraia na kuwa Mtanzania.
“Ni kweli hiyo picha ni yangu, na nilikuwa nimevaa jezi ya Yanga. Ilikuwa ni siku ya kawaida ya mazoezi binafsi. Nilikuwa gym, kiukweli siyo jambo la ajabu kuvaa jezi ya timu yoyote hasa kama ni zawadi au uliyobadilishana na mchezaji mwenzako,” alisema kiungo huyo anayehusishwa na Yanga.
“Mashabiki wana haki ya kuhoji, lakini ukweli ni kwamba mimi ni mchezaji wa mpira, napenda soka. Jezi sio lazima iwe ishara ya uhamisho. Wachezaji wengi huwa tunabadilishana jezi baada ya mechi. Nadhani hiyo haipaswi kuchukuliwa tofauti.”
Damaro, ambaye amekuwa mhimili wa safu ya kiungo katika kikosi cha Singida Black Stars, anaeleza kuwa tangu aanze maisha ya soka nchini, amekuwa na heshima kwa klabu kubwa kama Yanga.
“Nimecheza dhidi ya Yanga mara kadhaa, napenda mpira wao. Nimewahi kubadilishana jezi na mchezaji wao baada ya mechi, hiyo jezi niliivaa siku hiyo ya mazoezi. Sina ajenda yoyote nyuma ya hilo,” alisema.
Kuhusu tetesi kuwa huenda alikuwa katika mazungumzo na Yanga, Damaro alisema: “Sijaingia kwenye mazungumzo rasmi na Yanga, ila ni klabu nzuri kama ilivyo Simba. Hivi sasa niko na Singida, na nathamini kila kilichofanyika kati yangu na klabu yangu ya Singida.”