KIJIWE kimelinyooshea mikono gazeti la Mwanaspoti maana ndiyo lilikuwa chanzo cha kwanza kuripoti habari za ujio wa Romain Folz kuja kuwa Kocha Mkuu wa Yanga.
Ndicho kilichotokea kwani juzi Jumatano, Yanga ilimtangaza kocha huyo Msaidizi wa zamani wa Mamelodi Sundowns kuwa mrithi wa nafasi iliyoachwa wazi na Miloud Hamdi.
Hatujui Yanga imefikiria au imetazama vitu gani hadi ikaamua kumpa kazi hiyo Kocha Folz ambaye ana umri wa miaka 35 na japo hatuna kumbukumbu vizuri za huko nyuma, inawezekana akawa ndiye kocha aliyeweka rekodi ya kuinoa Yanga akiwa na umri mdogo zaidi.
Lakini hadi wameamua kukabidhi kikosi chao kwa Folz, hapana shaka wamejiridhisha ni mtu sahihi kwao kulingana na aina ya timu waliyonayo na malengo ambayo wamejiwekea kwa ajili ya msimu ujao wakiamini atawafikisha katika nchi ya ahadi.
Kuna fikra zimeibuka hapa kijiweni kuhusu ujio huo wa Folz na tunaona kama kocha huyo ndiye atanufaika zaidi na timu yake mpya aliyojiunga nayo kulinganisha na Yanga ambayo ndio muajiri wake.
Anajiunga na Yanga yenye kikosi bora zaidi na kipana chenye wachezaji wanaoweza kuiamua mechi kwa uwezo na juhudi zao binafsi, hivyo inaweza kumrahisishia kazi na akapata ushindi mara nyingi na kupandisha wasifu na thamani yake.
Ataifundisha timu inayopata sapoti kubwa nje ya uwanja kutoka kwa mashabiki, wanachama na viongozi jambo ambalo linaongeza ari na hamasa kwa wachezaji kujitoa vilivyo katika mechi za mashindano ili kuhakikisha timu inafanya vizuri.
Yanga ni timu ambayo ina historia nzuri ya kutwaa mataji ya ndani hivyo Folz anaweza kutembelea nyota hiyo na kuitumia kukuza jina lake ambalo kwa kiuhalisia halijulikani sana katika medani ya soka Afrika.
Hilo ni rahisi kufanikiwa kwa vile Watanzania hivi sasa tumekamata vilivyo mitandao ya kijamii hivyo Folz akifanikiwa Yanga, itakuwa ni rahisi sana kukuza jina lake kwa vile ataimbwa sana kuliko alipotoka.