ALIYEKUWA Kocha mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi aliyepo Ismailia ya Misri, amemchomoa mtaalam mmoja kutoka timu aliyowahi kufanya nao kazi ya Singida Black Stars.
Hamdi aliyeondoka Yanga mara baada ya kuwapa mataji mawili kwa mpigo ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA), mbali na lile la Kombe la Muungano aliwahi kuinoa Singida kwa muda mfupi kabla ya kutua Jangwani kuziba nafasi ya Saed Ramovic aliyenyakuliwa na CR Belouizdad ya Algeria.
Mtaalamu aliyechomolewa Singida ni kocha wa viungo wa timu hiyo, Marouene Slimani anayetarajiwa kuungana na Hamdi katika kikosi cha Ismailia.
Kocha huyo wa viungo tayari ameshawaaga wachezaji na viongozi wa timu hiyo na kuwatakia kila la kheri kwenye maisha mengine bila yeye.
Chanzo cha kuaminika kutoka Singida Black Stars kimeliambia Mwanaspoti kocha huyo mkataba aliokuwa nao umeshamalizika, pia ameshawishiwa na Hamdi aliyemleta nchini wakati akiinoa timu hiyo.
“Slimani alikuwa na Hamdi, isingekuwa rahisi kuendelea kusalia Singida Black Stars, hivyo tumemtakia kila la kheri aendako na sisi tunapambana kutafuta mbadala wake ili kujenga benchi la ufundi imara ambalo litaendana na kikosi kilichopo,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Baada ya kuondoka kwa kocha huyo, viongozi wamemfahamisha kocha mkuu ambaye anatarajia kuwasili mapema mwishoni mwa mwezi huu, kama atakuwa na mtu sahihi anayeweza kufanya naye kazi lakini na sisi pia tunapambana kutafuta.”
Mtoa taarifa huyo alisema timu yao imeshakuwa kubwa na makocha wengi wanatamani kufanya nao kazi hivyo haitakuwa kazi ngumu kupata mbadala sahihi ambaye atakuwa na malengo sawa na wao msimu huu ambayo ni kuhakikisha hawarudi nyuma baada ya kupata mafanikio ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu huu.