Karatu. Kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karatu umesaidia kuondoa adha ya baadhi ya wananchi wilayani humo, waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Julai 24, 2025 na baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi wilayani humo kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mmoja wa wananchi hao kutoka kijiji cha Changarawe, Wilfred Dahaye amesema kuwa awali walilazimika kutembea umbali wa kilomita 15, kutafuta huduma za afya katika kituo cha afya Karatu kabla ya kukamilika kwa hospitali hiyo ya wilaya.
Amesema hali iliyokuwa ikihatarisha maisha yao hususan kwa wajawazito na watoto wachanga.
“Uwepo wa hospitali hii umeleta nafuu na kuondoa changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati,” amesema
Naye Agness Jacob kutoka Kata ya Bashay, amesema awali walikuwa wakiteseka kufuata huduma hiyo ya afya umbali mrefu ila baada ya kukamilika wameondokana na changamoto.
“Kiukweli tulikuwa tukiteseka kupata huduma za afya hasa wanawake na watoto, ila tunashukuru Serikali kwa ujenzi wa hospitali hii ambayo ina vifaatiba vya kisasa,”amesema
Mganga Mkuu wa wilaya ya Karatu, Dk Hamisi Abdalla ameiomba Serikali kujenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa kilomita tano inmayotoka njia panda hadi hospitalini hapo kwani ni mbovu hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa.

Mganga huyo ametaja changamoto nyingine ni upungufu wa watumishi kwa asilimia 58, ambapo wana watumishi 89 huku mahitaji yakiwa 208.
“Changamoto nyingine ni ukosefu wa usafiri wa hii imepelekea watumishi wengi wanaoishi Karatu mjini, kulazimika kufuatwa na kurudishwa kila siku, hivyo kuongeza gharama za uendeshaji wa hospitali,” amesema.
Kihongosi amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi na kuwa ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu zaidi ya Sh4 bilioni.
Amesema ujenzi wa hospitali hiyo siyo tu umeongeza ufanisi kwa wilaya ya Karatu, bali pia kwa wilaya na mikoa jirani kutokana na uwepo wa vifaa vya kisasa.
Aidha aliwataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuepuka kutovunjiana heshima pindi wanapowajibishana.