INEC yawaonya wasimamizi kutobandika matangazo, orodha ya wapigakura

Mwanza. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewaonya waratibu na wasimamizi wa uchaguzi ambao hawatobandika mabango, matangazo na orodha ya majina ya wapigakura wakati wa uchaguzi, ikisema ni kinyume cha sheria na utaratibu wa uchaguzi.

Mjumbe wa INEC ambaye pia Jaji wa Mahakama Kuu,  Asina  Omari akifunga mafunzo ya siku tatu ya waratibu wa uchaguzi, wasimamizi, wasimamizi wasaidizi ngazi ya jimbo, maofisa uchaguzi na ununuzi leo Jumatano Julai 23, 2025 jijini Mwanza.

Akifunga mafunzo ya siku tatu ya waratibu wa uchaguzi, wasimamizi, wasimamizi wasaidizi ngazi ya jimbo, maofisa uchaguzi na ununuzi leo Jumatano Julai 23, 2025 jijini Mwanza, Mjumbe wa INEC ambaye pia Jaji wa Mahakama Kuu,  Asina Omari amesema changamoto ya kutobandikwa kwa majina hayo walikutana nayo maeneo mbalimbali waliyopita wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura.

“Tuliona changamoto ya kutobandikwa mabango yanayopaswa kubandikwa ili kuwaelekeza waliokuwa wana sifa ya yakuandikishwa na wadau wengine ili kujua mahali kilipo kituo,” amesema Jaji Asina.

Amewaelekeza kuwa suala la kutobandikwa matangazo na mabango lisitokee kwenye kituo cha uchaguzi badala yake yabandikwe kama inavyoelekezwa na sheria ya uchaguzi.

“Hivyo natumia nafasi hii kuwahimiza kuwa ubandikaji wa mabango, matangazo, orodha ya majina ni kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi ni wajibu wenu wa kuhakikisha mabango, matangazo, orodha ya majina na vyote vinavyotakiwa kubandikwa kulingana na kalenda ya utekelezaji wa majukumu ya uchaguzi yanafanyika ili kuepusha malalamiko ya ukiukwaji wa masharti ya sheria na kanuni za uchaguzi,” ameeleza.

Jaji Asina amewambia watendaji hao wa uchaguzi wakati wa utekelezaji wa majuku yao, watapaswa kutoa taarifa mbalimbali kwa vyombo vya habari ili kuhakikisha wananchi na wadau wanapata taarifa ya mambo mbalimbali kuhusu uchaguzi, lakini wajiridhishe na kuwashirikisha wenzao kabla ya kutoa taarifa hizo.

“Hakikisheni mnajiandaa kabla ya kukutana na vyombo vya habari, pima taarifa yako unayotaka kuitoa kabla hujaitoa ili kuepuka kuleta taharuki badala ya utulivu katika eneo lako na nchi kwa ujumla,” ameongeza.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya kusimamia na kuratibu uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025 yaliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Mwanza.

Ameendelea kuwasisitiza kutunza siri kama walivyoapa Julai 21, 2025 wakati wanaanza mafunzo hayo akisema endapo watatoa taarifa pasipo maelekezo ya tume watakuwa wametenda kosa.

“Kasimamieni mafunzo mliyofundishwa kwa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni na maelekezo ya tume. Pia, katoeni mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata na watendaji wa vituo vya kupigia kura kwa weledi,” amesema.

Mwenyekiti wa washiriki wa mafunzo hayo, Mujibu Babara amesema wamefundishwa mambo mbalimbali ikiwemo wajibu, majukumu na mambo mengine ya kuzingatiwa na waratibu, wasimamizi wa uchaguzi, makosa yanayofanywa na wasimamizi wa uchaguzi, urejeshaji wa fomu ya uteuzi na ukaguzi wake na namna ya kushughulikia kero za uteuzi.

“Tulielekezwa namna ya kuweka pingamizi na wanaoruhusiwa kuweka pingamizi pamoja na muda wake. Mada nyingine ilihusu maadili na kampeni za uchaguzi.

“Tulipitishwa kwenye kanuni za maadili, wanaohusika, yanayotakiwa kufanywa na wasimamizi na yasiyotakiwa kufanywa, yanayotakiwa na yasiyotakiwa kufanywa na wasimamizi wa vyama vya siasa, na yasiyotakiwa na yanayotakiwa kufanywa na Serikali,” amesema Babara.