Kocha Morocco aita mashabiki CHAN ’24

KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayojiandaa na fainali za michuano ya Ubingwa kwa nchi za Afrika (CHAN) 2024, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amewaita mashabiki kujitokeza katika mechi za fainali hizo akisema kikosi hicho kipo freshi kwa vita hiyo inayoanza Agosti 2-30.

Morocco aliyasema hayo mara baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Uganda The Cranes katika mechi ya michuano maalumu ya maandalizi ya fainali hizo za CHAN inayochezwa jijini Arusha na kusema kwa maandalizi ya kutosha iliyofanya, mashabiki wasiwe na wasiwasi na timu hiyo.

Tanzania imepangwa Kundi B sambamba na Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Afrika ya Kati na itafungua pazia Agosti 2 dhidi ya Burkina Faso kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Morocco alisema michuano hiyo ya Cecafa yanayoshiriki nchi tatu za Tanzania, Uganda na Senegal kwenye Uwanja wa Black Rhino uliopo Karatu ni msaada mkubwa kwa Stars kabla ya kuliamsha CHAN kama wenyeji sambamba na Kenya na Uganda.

Morocco alisema kikosi chake kwa sasa kimeimarika kutokana na maandalizi ambayo wamefanya kupitia kambi ya Misri, lakini mechi kadhaa ambazo walicheza kabla ya kujitosa katika fainali hizo za nane za CHAN tangu zilipoasisiwa mwaka 2009.

Ikiwemo mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Afrika Kusini na michuano ya soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) ambayo kwa namna moja ama nyingine imempa nafasi ya kuandaa vyema timu.

“Tanzania kila tukicheza mechi kuna mabadiliko makubwa yanakuwepo na hata mechi ya pili dhidi ya Senegal kutakuwepo na madaliko makubwa sana,” alisema Moroccco na kuongeza;

“Kikubwa kwa sasa ni kurebekisha makosa na kuendeleza yale mazuri kabla ya michuano ya Chan ambayo kwetu ni muhimu kutwaa ubingwa. Mshabiki wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono tukiwa kama wenyeji. Wajue wao ndio wachezaji wa 12 uwanjani.”