Timu 19 zilizogawanywa katika makundi manne zitashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) 2024 zitakazofanyika kuanzia Agosti 2 hadi 30 mwaka huu katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania.
Kundi A ambalo mechi zake zitachezwa katika nchi ya Kenya, linaundwa na wenyeji, Morocco, Angola, DR Congo na Zambia huku kundi B likiwa na wenyeji Tanzania, Madagascar, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mauritania na Burkina Faso.
Uganda ambayo ni mwenyeji mwenza imepangwa katika kundi C ambalo litakuwa pia na timu za Niger, Guinea, Algeria na Afrika Kusini na kundi D ambalo mechi zake zitachezwa Visiwani Zanzibar, litakuwa na Mabingwa Watetezi, Senegal, Congo, Sudan na Nigeria.
Historia ya mashindano hayo inafanya kundi B ambalo timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imepangwa, kutokuwa na mwenyewe au timu inayopewa nafasi kubwa kutamba kutokana na zote tano zilizo katika kundi hilo kutokuwa na historia ya mafanikio makubwa kwenye mashindano hayo.
Ni Madagascar pekee ambayo angalau inaweza kuweka kifua mbele kwani imewahi kumaliza katika nafasi ya tatu mara moja ambayo ilikuwa ni fainali za 2022, Afrika ya Kati inashiriki kwa mara ya kwanza, Mauritania imewahi kuishia robo fainali mara moja, Burkina Faso imewahi kushiriki mara tatu nyuma na kukwamia hatua ya makundi kama ilivyo kwa Tanzania ambayo ilishiriki fainali hizo mara mbili tofauti hapo nyuma.
Wenyeji wengine wa fainali hizo, Kenya ‘Harambee Stars’ wanaonekana kuwa katika kundi la mtego kutokana na kukutanishwa na timu nyingi zilizowahi kufanya vizuri kwenye mashindano hayo katika nyakati tofauti.
Kenya itakuwa na mabingwa wawili wa kihistoria wa mashindano hayo ambao ni Morocco na DR Congo ambazo kila moja imewahi kutwaa taji la CHAN mara mbili, kuna Angola ambayo imewahi kumaliza katika nafasi ya pili mara moja na mara moja kuishia robo fainali huku pia ikiwepo Zambia ambayo imewahi kushika nafasi ya tatu katika mashindano hayo mara moja na kuishia robo fainali mara tatu kati ya nne ilizoshiriki.
Wakati timu nyingine nne kwenye kundi hilo zikiwa na uzoefu na historia ya kutamba, Kenya yenyewe ndio inashiriki kwa mara ya kwanza fainali za CHAN.
Uganda katika mtego wa rekodi
Uganda ndio timu kutoka Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) iliyoshiriki Fainali za CHAN mara nyingi ambapo imefanya hivyo mara sita kati ya saba zilizopita lakini awamu zote hizo imeishia hatua ya makundi.
Hakuna timu iliyowahi kutwaa ubingwa kwenye kundi lake lakini wapinzani wake wote wana mafanikio ya kutambia kwenye CHAN kulinganisha na wao.
Algeria imewahi kufika hatua ya fainali, Afrika Kusini inajivunia kufika robo fainali mara moja, Guinea imeshamaliza katika nafasi ya tatu mara moja huku Niger ikiwahi kumaliza katika nafasi ya nne mara moja.