Mabilioni ya misaada ya USAID yafutwa rasmi

Dar es Salaam. Bunge la Marekani limekamilisha hatua ya kulivunja rasmi Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), baada ya kurejeshwa kwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya misaada ya kibinadamu, huku Tanzania ikieleza hatua ilizochukua mpaka sasa.

Hatua hiyo inatokana na kufungwa rasmi kwa shirika hilo Julai mosi, 2025, kufuatia maagizo yaliyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, alipoingia madarakani Januari 20, 2025.

Uamuzi wa Ikulu ya Marekani kufuta misaada hiyo ulipingwa mahakamani kwa misingi ya Katiba, ambayo inatamka kuwa ni Bunge pekee lenye mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya fedha za umma, haki inayojulikana kama Power of the Purse.

Kwa kuhalalisha hatua za Ikuluzilizofanywa bila idhini ya Bunge, Congress imeipa Rais wa Marekani sababu mpya ya kusherehekea.

Kura ya mwisho iliyopigwa katika Seneti Julai 17, imemaliza rasmi uwepo wa USAID ambalo lilikuwa lengo la kwanza la Trump aliposhika urais.

Julai 23, wabunge wa Marekani walirejesha serikalini Dola bilioni 9 (sawa na Sh23.3 trilioni) ambazo tayari zilitengwa kwa ajili ya mashirika ya kibinadamu, hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu mwaka 1999.

Kwa kutumia mchakato adimu wa kisheria uitwao rescission (yaani kufuta matumizi yaliyopitishwa), Baraza la Wawakilishi na Seneti wameandika katika sheria hatua za kupunguza bajeti ya misaada ya kimataifa, kama ilivyopendekezwa na Rais Trump na Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE) inayoongozwa na Elon Musk.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeliarifu Bunge kuwa itachukua baadhi ya majukumu ya USAID kama sehemu ya mabadiliko ya kiutendaji. Mipango ambayo haikidhi vipaumbele vya utawala wa Trump itafutwa.

“Tunaelekeza upya programu zetu za misaada ya kigeni ili ziendane moja kwa moja na maslahi ya Marekani na wananchi wake,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio.

Kufuatia uamuzi huo, leo Alhamisi, Julai 24, 2025, Mwananchi limezungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa Tanzania, Dk Seif Shekalaghe, aliyesema kusitishwa kwa misaada hiyo hakuna kitu kitakachokwenda tofauti, kwani Serikali ina wajibu wa kuhudumia wananchi na hakuna huduma itakayotetereka.

“USAID ilitoa mchango wake lakini haikuwa kwa asilimia 100, walikuwa wanaisaidia Serikali. Mpaka sasa wadau wote tunaoshirikiana nao wanachangia. Hata wanapoondoka, Serikali inaendelea kutekeleza. Walikuja wakaingia na kusaidia, tutaendelea kama kawaida kuhudumia wananchi,” amesema.

Dk Shekalaghe amesema Serikali imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na wadau wa nje na ndani.

Hata hivyo, bado watumishi wa afya zaidi ya 13,000 waliokuwa wamesitishwa katika hospitali mbalimbali nchini kutokana na kusitishwa kwa misaada ya USAID hawajarejea kazini tangu kusitishwa kwa ajira zao Januari 2025.

Watumishi hao walikuwemo madaktari, wauguzi walioajiriwa vituo kadhaa, wataalamu wa ustawi wa jamii, wataalamu wa maabara, maofisa miradi wanaofanya tathmini ya miradi, wahasibu, wanaoshughulika na ugavi, wafanyakazi wa kada ya kati ya tiba, matabibu na wengineo.

Karibu kila kada kwenye afya ilipata nafasi ya kufanya kazi kwenye miradi mbalimbali inayohusishwa na USAID au PEPFAR.

Alipoulizwa kuhusu kuondoka kwa watumishi wa afya waliolipwa mishahara na mashirika mbalimbali yaliyopokea misaada kutoka USAID, Dk Shekalaghe amesema: “Bado hatujapokea taarifa kwamba huduma zimeshindikana kutolewa, kazi zinaendelea kama kawaida.”

Mapema mwaka huu, Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2025/2026 imeanzisha vyanzo vya mapato nane kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya ukimwi na kugharamia bima ya afya kwa wote.

Hatua hizo zilitajwa kuwa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh586 bilioni.

Juni 12, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni, Mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/2026 alisema hatua hizo zimefuatia mabadiliko ya kisera yanayoendelea duniani, ambayo yamesababisha wadau muhimu wa maendeleo kupunguza misaada iliyokuwa inatolewa kwa ajili ya huduma za afya, ikiwemo kukabiliana na kudhibiti magonjwa mbalimbali hususan Ukimwi.

Alisema Serikali inapendekeza kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato, ili kupunguza nakisi ya kibajeti iliyotokana na kupungua kwa misaada hiyo kwa kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali.

“Inapendekezwa asilimia 70 ya mapato yatakayoongezeka ipelekwe kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) na asilimia 30 ipelekwe kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote,” alisema.

Akitaja marekebisho hayo, Mwigulu alisema serikali itafanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 ili kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kilevi vinavyozalishwa na vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi.

Alisema Sh20 kwa lita kwa bia zinazotambulika kwa Heading 22.03, Sh30 kwa lita kwa mvinyo unaotambulika kwa Heading 22.04, 22.05, na 22.06 Sh50 kwa lita kwa pombe kali na vinywaji vingine vinavyotambulika kwa Heading 22.08.

Marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 ili kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya kielektroniki kutoka asilimia 17 hadi asilimia 17.5.

Marekebisho mengine ilikuwa kuanzisha tozo katika mafuta, madini, Michezo ya kubahatisha, kwenye michezo ya kasino, magari na mashine zinazoingizwa kutoka nje, pia Sh250,000 kwa mashine (Excavators, Bulldozers, Fork Lifts) zenye Heading 84.29 na 84.27.

“Pia kutoza Sh500 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya treni na kutoza Sh1000 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya anga,” alisema.

Kufuatia hilo, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimesema Serikali inapaswa kuangalia namna ya kuongeza rasilimali watu katika maeneo ambayo wafanyakazi hao wameondoka.

“Bado wananchi wanataka huduma. Kufungwa kwa shirika ni kweli kuna athari za moja kwa moja. Kwanza imekuwa ghafla, pili tulikuwa hatujazoea. Sasa wengi wamepoteza ajira. Hili halitadumu milele, tutasimama tena, sijui ni kwa muda gani,” amesema Rais wa MAT, Dk Mugisha Nkoronko.

Amesema wanaishauri Serikali kuona namna inavyoweza kuingilia kati ili waendelee kutoa huduma kwenye vituo vilivyokuwa vimetengwa.

Pia amesema kujiondoa kwa Marekani bado Watanzania wanahitaji huduma, zikiwemo za VVU na Ukimwi, magonjwa ya kuambukiza, chanjo, huduma za lishe na nyinginezo.

“Zile huduma zilikuwa za muhimu, hazibadiliki. Kwa vile Marekani imejiondoa bado watu wetu wanahitaji huduma. Tuliona Serikali ilianzisha vyanzo vinane kushughulikia VVU na huduma nyingine za afya, ikiwemo Bima ya Afya kwa Wote.

“Hatutaki kiwe kitu cha muda mfupi. Hii ni kengele ya kutuamsha: mtegemea cha nduguye hufa masikini. Lazima tuangalie tunaondoka vipi hapa tulipo. Na kwenye mipango ya Serikali si kwamba milango yote imefungwa; tunaweza kuangalia mashirika mengine ya nje tunayoweza kushirikiana nayo,” amesema Dk Mugisha, ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya upasuaji katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Kwa upande wake, mshauri na mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati, amesema Marekani imekuwa na mchango mkubwa kwenye asasi na mashirika mengi nchini yanayoshughulikia elimu, afya na mazingira. Hivyo, kujitoa kwa Marekani kunatuamsha kujitegemea.

Dk Osati amesisitiza nchii ijipange: “Tunatakiwa tujiimarishe sana ndani. Tuna Mfuko wa ATF lakini hatujawahi kuelekeza nguvu eneo hilo. Pia kwenye bara letu la Afrika tuweze kushawishi mataifa makubwa kama China kuwekeza fedha nyingi WHO.”

Mpaka mwaka 2025, orodha ya miradi ya USAID ambayo imekuwa ikitekelezwa nchini ni pamoja na kilimo na upatikanaji wa chakula, demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, ukuaji wa uchumi na biashara, elimu, mazingira, jinsia na vijana pamoja na afya.

Kwa mwaka 2023 pekee, USAID ilitoa zaidi ya Dola milioni 400 za Marekani kama ruzuku ili kuimarisha biashara, kukuza ajira, na kuchochea maendeleo nchini Tanzania.

Shirika la USAID lilianzishwa mwaka 1961 na Rais John F. Kennedy, huku ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania ukidumu kwa zaidi ya miongo sita.

Hata hivyo, nchi 132 ambazo zilikuwa zikinufaika moja kwa moja na ufadhili kutoka kwa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), ziko hatarini kupoteza jumla ya watu milioni 14 kufikia mwaka 2030 baada ya kufungwa rasmi kwa shirika hilo la kutoa misaada.

Utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la sayansi la Lancet unaeleza kwa kina jinsi hatua zilizopigwa katika miongo miwili iliyopita kupunguza vifo vya watoto na watu wazima, zinavyoweza kuporomoka kufuatia hatua hiyo.

“Makadirio yetu yanaonyesha kuwa, kama hatua za kupunguza ufadhili zilizotangazwa na kutekelezwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025 hazitaondolewa, idadi kubwa ya vifo vinavyoweza kuepukika vinaweza kutokea kufikia mwaka 2030,” wamesema watafiti.