Dodoma. Serikali imeweka mkakati wa kila eneo litakalokuwa na mgodi mpya wa uchimbaji madini, litenge sehemu maalumu kwa ajili ya kuwapatia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Julai 24, 2025 na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Ali Samaje wakati akifungua semina ya mafunzo kwa wanawake wachimbaji wadogo ambayo inalenga kuwajengea uwezo na kuwasaidia vifaa na vitendea kazi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameratibiwa na mtandao wa Tanzania Women in Mining and Mineral Industry (TWIMMI) kwa kushirikiana na Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), ambapo wamewakutanisha wanawake kutoka mikoa mbalimbali wakiwemo maofisa na makamishina wa madini wanawake.
Samaje amesema lengo la Serikali ni kuona wanawake wanakuwa kiuchumi na kazi ya kuchimba, kuchenjua, kuongeza thamani katika madini hata biashara kwa ujumla siyo ya wanaume pekee.
Amesema Serikali imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa kuwainua wanawake kwenye makundi tofauti tofauti, ndiyo maana wamegeukia kundi la wachimbaji madini ili kuwajengea uwezo nao wajione wako sawa na watu wengine katika shughuli zao.
“Hilo limeshapitishwa na linatekelezwa, tunaamini kuwa ukimwezesha mwanamke unakuwa umeinua uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla, lakini uchumi wa wanawake, vijana na wenye ulemavu ukikuwa hapa pato la nchi huongezeka,” amesema Samaje.
Akizungumzia mafunzo hayo, Samaje ambaye ni Kamishina Msaidizi wa Migodi na Machimbo amesema yanawajengea uwezo wa kutambua juu ya thamani yao na kwamba yatakuwa na msaada mkubwa katika kuwatia moyo hasa vifaa na vitendea kazi wanavyopatiwa.
Katibu wa TWIMMI, Mecktilder Mchomvu amesema lengo la mkutano huo ni kuwajengea uwezo wanawake wachimbaji wadogo pamoja na makundi maalumu ikiwemo wenye ulemavu.
Mchomvu amesema hadi sasa jumla ya wanawake 3,900 wamefikiwa na mpango huo ambao umegusa nchi nzima licha ya kuwa katika eneo la ugani. Amesema wamejielekeza zaidi mikoa ya Dodoma, Morogoro, Singida na Tanga na ndiko walikoanzia kutoa ujuzi.
Katibu huyo amesema hakuna jinsi unavyoweza kuwakwepa wanawake katika maarifa na mpango wa ukuzaji uchumi, kwani wako karibu zaidi na jamii na wanaendelea kuwa sehemu ya watu muhimu, ndiyo maana waliamua kujikita katika kundi hilo.
Mwakilishi wa UNDP nchini, Geofrey Nyamlunda amesema mbali na fursa walizonazo wanawake, wanakabiliwa na changamoto kwenye shughuli hizo ikiwemo kudharauliwa na kuhisiwa kuwa hawawezi kufanya kazi ya madini.
“Tumejikita kwenye eneo hili kwani tunatambua kundi la wanawake wamekuwa ni watu wa kubezwa, kwamba hawawezi kufanya chochote, kuwa na thamani kubwa katika utendaji wao na huenda hawawezi hata kuwa na mbinu za kuongeza thamani katika shughuli hii ya madini, lakini sasa wameonekana ni kundi lililokuwa limeachwa na ujuzi wao kutoonekana,” amesema Naymlunda.
Amesema tangu mwishoni mwa miaka 1970, UNDP ilianza kuwa karibu na wanawake kwenye miradi mingi, jambo lililozaa matunda kwa kiasi kikubwa na tija imeonekana ambapo changamoto zao zimekuwa zikipungua siku hadi siku.