Dar es Salaam. Leo Julai 24, 2025, Watanzania wanatimiza miaka mitano tangu kumpoteza Rais mstaafu wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa, kiongozi aliyesifika kwa busara, uchapakazi, na kauli zake zilizobeba ujumbe mzito kwa Taifa.
Mkapa alifariki dunia Julai 24, 2020 na alizikwa Julai 29, 2020 kijijini kwao Lupaso mkoani Mtwara.
Mkapa anakumbukwa kwa msemo wake maarufu: “Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe,” kauli iliyowahamasisha Watanzania kujitegemea, kuthamini kazi na kuwa na ari ya maendeleo.
Pia, alipunguza umbali kati ya kiongozi na raia kwa kutumia salamu yake ya ‘mambo?’ na wananchi walijibu kwa kusema ‘poa’, jambo lililobeba hisia za ukaribu na ushawishi wa mawasiliano.
Hayati Mkapa katika miaka yake mitano ya kumbukizi, mchango wake katika ujenzi wa Taifa unaendelea kuthaminiwa kutoka kwenye mageuzi ya kiuchumi, uimarishaji wa taasisi za umma hadi kukuza diplomasia ya kimataifa kwa Tanzania. Urithi wake bado unaishi mioyoni mwa Watanzania.

Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania, hayati Benjamin Mkapa enzi za uhai wake.
Si hivyo tu, hayati Mkapa anakumbukwa kwa hotuba zake zilizobeba uzito wa fikra, ujasiri wa kisiasa na uchambuzi wa kina wa masuala ya kitaifa na kimataifa.
kwa kutumia lugha fasaha, iliyopambwa na nukuu kutoka kwenye vitabu vya fasihi maarufu duniani, hasa vya William Shakespeare, jambo lililomtofautisha na viongozi wengi wa wakati wake.
Hotuba zake hazikuwa tu taarifa kwa umma bali pia zilikuwa nyenzo za kuelimisha, kuhamasisha na kuchochea fikra mpya kwa Taifa.
Alizungumza kwa uthubutu, akigusa masuala nyeti bila kuyapapasa, huku akitumia marejeo ya kihistoria na kifalsafa kuonyesha uzito wa ujumbe aliotaka kuwasilisha.
Kwa wengi, hotuba za Mkapa ziliwafungua macho na kuwa darasa lisilo rasmi la uongozi, uzalendo na maadili ya utumishi wa umma.
Mfano wa hotuba ya Mkapa ni ile aliyoitoa katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM, uliofanyika Dodoma Agosti 25, 2004, iliyokuwa mfano wa ujasiri na uthubutu wa kweli wa kiuongozi.

Katika hotuba hiyo maarufu, Mkapa alianza kwa kusema kwa msisitizo:
“Leo nimeamua kutoa hotuba, tena iliyoandikwa, maana jambo nitakalolizungumza ni zito na nimelitafakari kwa muda sasa. Napenda kuzungumza nanyi kuhusu ushupavu wa uongozi, kwa Kiingereza: ‘The Courage of Leadership.’
Kauli hiyo peke yake ilionesha namna alivyotambua uzito wa ujumbe aliotaka kuwasilisha kwa chama chake na kwa Taifa.
Alikuwa kiongozi aliyekuwa tayari kusema ukweli hata kama ulikuwa mchungu kwa lengo la kulinda misingi ya haki, uwajibikaji na uadilifu ndani ya chama na Serikali.
Mkapa kupitia hotuba yake aliwaalika viongozi wa CCM kutafakari kwa kina kuhusu ujasiri unaohitajika kuongoza Taifa: ujasiri wa kufanya maamuzi sahihi bila kuyumbishwa na vishawishi vya kisiasa, ujasiri wa kusimamia maadili, na ujasiri wa kukemea rushwa na ufisadi mambo ambayo wakati huo yalikuwa yanatikisa jamii.
Pia, alisisitiza maandalizi ya kina kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, akitaka chama kijitathmini, kijirekebishe na kizingatie taratibu na maadili yake.
Kwa mtazamo wake, ushindi wa CCM si kwa sababu ya nguvu ya chama pekee, bali kwa kuandaa viongozi bora wenye maadili na uwezo wa kweli.

“Chama imara kinapaswa kuwa na wagombea imara, wenye sifa, uwezo na ushupavu,” alisema, akiweka wazi kuwa kutegemea nguvu ya chama bila kujijenga binafsi ni hatari inayoweza kuua ubora wa viongozi na hatimaye kuathiri nchi nzima.
Mkapa anakumbukwa kwa namna alivyojizatiti kujenga mifumo imara, kuboresha maisha ya wananchi, na kuimarisha demokrasia na ustawi wa taifa.
Miongoni mwa mambo Mkapa anakumbukwa ni kuanzia mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria.
Kabla ya Mkapa kuingia madarakani, Tanzania ilikuwa inakabiliwa na changamoto kuhusu matumizi ya maji ya Ziwa Victoria.
Nchi kama Misri, ambazo ni washirika wa mkataba wa zamani wa kikoloni kuhusu ugawaji wa maji hayo kupitia Mto Nile, zilizuia Tanzania kutumia maji ya ziwa hilo kikamilifu.
Mkataba huo wa zamani uliwapa Misri na nchi nyingine sehemu kubwa ya haki za matumizi ya maji ya Mto Nile, ikiwemo Ziwa Victoria, hali ambayo ilisababisha Tanzania kushindwa kupata haki zake kamili za kutumia rasilimali hii muhimu kwa maendeleo.

Rais Mkapa alipokuwa madarakani, alikataa kwa uthubutu hali hii ya kunyanyaswa na mikataba ya zamani.
Alitoa idhini ya ujenzi wa miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria bila ya kuogopa kupingana na misimamo ya Misri.
Hatua hii ya ujasiri ilifungua mlango kwa Tanzania kutumia rasilimali za maji za Ziwa Victoria kwa maendeleo yake, ikileta nafuu kubwa kwa wakazi wa maeneo yaliyokuwa yanakabiliwa na uhaba wa maji.
Mkapa alianzisha Mpango Maalumu wa Elimu ya Msingi (MMEM), na mipango mingine ka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa ajili ya kuzisaidia kaya maskini kupata huduma za msingi na kujikwamua kiuchumi.
Katika sekta ya afya, mafanikio yalionekana kwa kasi kupitia uboreshaji wa miundombinu na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa kama vile mashine za X-Ray, sambamba na uwepo wa dawa muhimu katika hospitali nyingi za wilaya. Mageuzi haya yaliimarisha huduma za afya na kupunguza pengo la upatikanaji wa matibabu kati ya mijini na vijijini.
Pia, Mkapa alianzisha Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (Mkurabita) kwa lengo la kuwawezesha wananchi wanaojishughulisha na biashara ndogondogo kuingia katika mfumo rasmi wa uchumi, kuongeza fursa za mikopo, ulinzi wa mali na ustawi wa kiuchumi.

Katika harakati za kuwatoa Watanzania katika umaskini, Mkapa alimwalika nchini mchumi mashuhuri kutoka Peru, Profesa Hernando de Soto, kiongozi wa taasisi binafsi ya The Institute for Liberty and Democracy (ILD).
Kupitia taasisi yake ya ILD, de Soto alikuja nchini mwaka 2003 kwa ajilia ya kusaidia kuibua sera bunifu za kiuchumi zitakazowasaidia Watanzania hasa wale wa kipato cha chini kuinuka kutoka kwenye umaskini.
Lengo kuu lilikuwa kuchochea mchakato wa kurasimisha rasilimali na mali za wananchi wa kawaida, kwa imani kuwa kumiliki mali rasmi kungefungua milango ya upatikanaji wa mikopo, biashara na ustawi wa kiuchumi.
Kuboresha Jiji la Dar es Salaam
Mkapa alipoingia madarakani, Jiji la Dar es Salaam lilikuwa na hali mbaya kutokana na uchafu, uchakavu wa miundombinu. Hivyo alivunja uongozi wa Jiji la Dar es Salaam na kuunda Tume iliyokuwa chini ya mwenyekiti Charles Keenja.
Tume hiyo ilitambulika kama Tume ya Keenja ilifanya kazi kubwa yenye kukumbukwa, ikasafisha jiji, na kukarabati majengo mbalimbali ya Serikali na jiji likaanza kuwa na mwonekano mpya.
Kabla ya hapo ilikuwa ni kawaida kwenda kwenye mitaa ya Posta na kukuta vinyesi pembezoni mwa majengo mbalimbali.
Mfumo wa Serikali kiuchumi
Mkapa pia alifanya mageuzi ya kimfumo katika Serikali yaliyolenga kuweka misingi imara ya utawala bora na maendeleo endelevu.
Mojawapo ya hatua alizochukua ilikuwa ni kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa kuanzisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), hatua iliyosaidia kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza utegemezi wa misaada ya nje.
Aidha, alianzisha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa lengo la kulinda haki na ustawi wa wafanyakazi baada ya kustaafu, sambamba na kuboresha utendaji kazi wa Serikali za Mitaa kupitia Ofisi ya Rais–Tamisemi, ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi moja kwa moja.
Miongoni mwa mafanikio ya muda mrefu ya utawala wake ni uanzishwaji wa taasisi muhimu kama vile Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
Mifumo hii ya kitaasisi imeendelea kuwa nguzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi hadi leo, na ni sehemu ya urithi mkubwa aliouacha kwa Taifa.
Mkapa pia atakumbukwa kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati iliyobadili sura ya Taifa kwa namna ya kipekee.
Alijenga Uwanja wa Taifa (sasa Benjamin Mkapa Stadium), mojawapo ya viwanja vya kisasa zaidi barani Afrika, ambao umechangia kukuza michezo na kuongeza heshima ya nchi kimataifa.
Pia, alisimamia ujenzi wa Daraja la Mkapa lililounganisha mikoa ya kusini na kaskazini, na kupunguza kwa kiasi kikubwa adha ya usafiri, biashara na usambazaji wa huduma.
Daraja hilo si tu lilikuwa la kimkakati kiuchumi, bali pia alama ya dhamira yake ya kuunganisha Watanzania.
Mkapa pia alianzisha Tume ya Taifa ya Kupambana na Ukimwi (TACAIDS), taasisi muhimu katika mapambano dhidi ya janga la Ukimwi, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kulinda afya za wananchi na kudhibiti maambukizi mapya.
Miradi hii na taasisi alizoziasisi zimeendelea kuwa nguzo imara za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini, zikionesha kwa vitendo namna alivyoweka misingi endelevu kwa vizazi vijavyo.