Mashahidi 13 kutoa ushahidi kesi ya wizi wa Sh3.4 bilioni

Dar es Salaam. Mashahidi 13 na vielelezo 20 vinatarajiwa kutolewa mahakamani katika kesi ya kujipatia Sh3.4 bilioni kwa njia ya udanganyifu inayomkabili Mkurugenzi na mwanahisa wa duka la kubadilishia fedha la Fx Bureau De Change, Faruk Sidick.

Sidick anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia Sh3.4 bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha kinyume cha sheria.

Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama Kuu, pindi kesi hiyo itakapopangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa, baada ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Edger Bantulaki ameieleza mahakama hiyo, leo Alhamisi Julai 24, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, wakati akimsomea mshtakiwa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Kabla ya kuwasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo, Wakili Bantulaki alimkumbusha mshtakiwa mashtaka yake na kisha kumsomea upya.

Alidai mshtakiwa anadaiwa kati ya Agosti 28 na Novemba, 2018, eneo la Samora wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai alijipatia Sh3.4 bilioni.

Inadaiwa fedha hizo alizipata kutoka Roshanal Moledina, baada ya kumdanganya kuwa atazibadilisha kuwa dola za Marekani 1,550,000, sawa na Sh3.4 bilioni, huku akijua siyo kweli.

Katika shtaka la pili, siku na eneo hilo mshtakiwa anadaiwa kutakatisha fedha hizo, wakati akijua wazi kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Inadaiwa kuwa mlalamikaji (Melodina) anamiliki duka la vifaa vya pembejeo.

Na Agosti 28, 2028, mshtakiwa alikutana na mlalamikaji na kumshauri kuwa fedha zake azibadilishe kutoka fedha za Tanzania hadi kuwa dola za Marekani, ili ikifika kipindi cha kilimo, akanunue vifaa vya kilimo nchini India.

Hivyo, mshtakiwa huyo alimtaka Melodina kuzipeleka fedha hizo katika duka lake la kubadilishia fedha la Fx Bureau De Change, lililopo Samora ili zibadilishe na kuwa dola za marekani, ili muda ukifika wa kwenda India iwe rahisi kuzichukua na kwenda kufanyia manunuzi za vifaa vya kilimo.

“Mlalamikaji alikubaliana na wazo la Sidick na akawa kila siku wakiuza katika duka lake, jioni pesa hizo za mauzo wanazipeleka katika duka la hilo na wanaandikishiana katika daftari na kusaini” alidai wakili.

Wakili Bantulaki alidai kuwa mlalamikaji alifanikiwa kuweka dola za Marekani 1,550,000.

Hata hivyo, ulipofika msimu wa kilimo, Moledina alikweda kwa Sidick kuchukua fedha zake, lakini mshtakiwa huyo alimwambia hana pesa.

Baada ya muda, hakuonekana na walivyofuatilia walieleza kuwa maduka yake ya kubadilishia fedha yamefungiwa na Serikali.

Kutokana na hali hiyo, mhasibu wake alimshauri wakae vikao vya familia na kuzungumza namna watakavyomlipa.

“Lakini baadaye, mhasibu alimshauri mlalamikaji aende Kituo cha Polisi akaripoti suala hilo kwani limekuwa gumu,” alidai.

Melodina alienda kituo cha Polisi na kutoa taarifa ya wizi wa fedha zake na baada ya hapo, mshtakiwa alikamatwa na baada ya uchunguzi kukamilika alifikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Magutu alimwambia mshtakiwa kuwa kesi yake ameihamishia Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji, na wakati akisubiri kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuanza kusikilizwa Sidick atakuwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.