Matunda baada ya maonyesho Sabasaba 2025

Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba (DITF), yaliyofanyika mwaka 2025, yameweka historia kwa kuwa jukwaa lenye mvuto wa uwekezaji, ubunifu wa teknolojia na ushirikiano wa kimataifa.

Upekee wa Sabasaba ya mwaka huu umejidhihirisha katika idadi kubwa ya washiriki ambao walikuwa zaidi ya 3,500 kutoka ndani na nje ya nchi na uwepo wa mataifa 23 yaliyokuja kuonyesha teknolojia, bidhaa na huduma mpya.

Maonyesho ya Sabasaba ambayo yalifikia tamati Julai 13 mwaka huu, yalifunguliwa rasmi Juni 28 huku biashara ya zaidi ya Sh7.06 bilioni ikifanyika na oda za zaidi ya Sh44.4 bilioni zikitolewa kwa wauzaji mbalimbali.

Kwa mara ya kwanza, Sabasaba ilijikita katika kuendesha mambo yake kidijitali ikiwamo kuanzia hatua za awali za watu kuchagua mabanda kwa njia ya mtandao na kufanya malipo bila kuwa na ulazima wa kufika uwanjani.

Hilo lilienda sambamba na kurekodi idadi ya watembeleaji waliofika uwanjani hapo kila siku hali iliyoweka urahisi katika utunzaji wa kumbukumbu lakini je, nini kinafuata baada ya maonyesho hayo.

Moja ya sehemu iliyopamba maonyesho haya ilikuwa ni ubunifu kutoka kwa wanafunzi mbalimbali wa vyuo vikuu nchini ambao walionyesha namna teknolojia inavyoweza kurahisisha na kutatua changamoto za jamii inayowazunguka.

Bunifu hizo zilizovuta hisia za watu wengi, zilifanya wananchi kutaka ziendelezwe kwa haraka ili ziweze kuwasaidia katika majukumu yao ya kila siku ikiwamo zile zilizohusu kilimo.

Hata hivyo baadhi ya bunifu zimerudishwa uwanjani hapo kwa miaka mitatu hadi minne mfululizo huku kukosekana kwa ufadhili wa kuziendeleza ukitajwa kuwa sababu.

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ilizungumzia suala hilo huku ikikiri kuwa mara zote wamekuwa wakipita katika maonyesho hayo na kukagua bunifu ambazo wanaweza kuziendeleza.

Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu alipozungumza na gazeti hili anasema kwa bahati mbaya kumekuwa na bunifu nyingine ambazo haziendelezeki.

Hiyo ni kwa sababu mlaji wa mwisho wa ubunifu wowote ni mwananchi ambaye ndiye anapaswa kuona tija ya uwepo wa ubunifu huo na kama hautamgusa basi itakuwa ni ngumu kuuendeleza.

“Kuna baadhi ya wabunifu ukiwaambia ubunifu wake hauna tija hawezi kukuelewa kwa sababu anakuwa amejiamini. Mlaji hayupo kuna bunifu nyingine ni kwa ajili ya kuonyesha kuwa amejifunza na kuelewa lakini si kwa ajili ya kwenda sokoni kwa sababu nani atalipia ubunifu huo au utasaidiaje watu,” anasema.

Anasema watu wanapaswa kutambua kuwa ubunifu ni kitu ambacho hakipo au kama kipo basi kimeongezwa vitu zaidi, lakini isiwe mwaka jana alifadhiliwa mtu akiwa na ubunifu fulani na mwaka huu anakuja mtu mwingine na kitu kilekile akitaka ufadhili kwa sababu tu aliyepewa hela alitoka Mwanza na yeye ametoka Mbeya.

Amesema Costech imekuwa haitoi mtaji bali kianzio ili wabunifu waweze kuboresha kile walichokifanya na kwenda sokoni lakini baadhi yao wamekuwa wakishindwa kutokana na tija ndogo iliyopo katika bunifu.

“Ndiyo maana huwa tunasisitiza wabunifu kwenda kwenye maonyesho mbalimbali ili waone wenzao wanafanya nini katika bidhaa kama hizo,” anasema Dk Nungu.

Katika uendelezaji wa bunifu hizo pia vyuo vimejipanga kuwawezesha wanafunzi wake ikiwamo Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere chenyewe kilichoamua kuja na sera ambayo itawezesha uendelezaji wa bunifu za wanafunzi wake ili ziweze kuingia sokoni na kuleta tija.

Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Haruni Mapesa anasema wanazo bunifu zaidi ya 30 za wanafunzi ambazo wanazipata katika taaluma zao, nyingi zikiwa upande wa Tehama hivyo waliona ni vyema kutafuta namna ya kuziendeleza.

“Katika fedha hizo pia tunaweka mkakati wa kuwaunganisha na taasisi zinazosajili hakimiliki ya bunifu zao ili waweze kuziingiza katika biashara. Sera hii inatoa mwongozo wa namna ya kuendeleza mawazo yao na kuwaunganisha na wafanyabiashara,” anasema Profesa Mapesa.

Alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara wanaotaka kutumia bunifu hizo ili ziweze kuingia katika biashara.

“Kama chuo tumejipanga kuwasaidia kuboresha mawazo na kuwaunganisha na wadau wanaoweza kuwasaidia kukamilisha kazi zao na kuwanufaisha katika kuwapa mapato kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Amesema kama chuo wanasimamia mkakati wa kuwaendeleza wabunifu kwani wanaamini watasaidia katika kupunguza changamoto ya ajira kupitia kujiajiri na kuajiri wenzao.

“Sisi kama wataalamu tunawatia moyo kwani kila wanapoanza siyo kwamba wanafaulu mara moja ndiyo maana tunawaongoza ili wasikate tamaa katika bunifu zao,” amesema.

Baada ya biashara ya zaidi ya Sh7.06 bilioni kufanyika na oda za zaidi Sh44 bilioni kutolewa imesisimua zaidi hamasa ya wafanyabiashara huku utafutaji wa masoko mapya ya bidhaa za tanzania ndiyo jambo ambalo linafanyika kwa sasa.

Hilo linafanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoyatoa wakati akifunga maonyesho ya 49 ya Sabasaba.

Majaliwa aliitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kuongeza nguvu katika kutafuta masoko ya ndani na nje ili wanaoleta bidhaa katika maonyesho hayo wawe wanajua nini wanauza, hali itakayosaidia upatikanaji wa fedha zaidi za kigeni.

“Eneo Huru la Biashara Afrika (AFTCA) na Soko la Sadc (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika), ni masoko yenye ushindani hivyo ni vyema uchambuzi wa kina ukafanyika wa masoko hayo ili kujua bidhaa ambazo zinaweza kuuzwa na wafanyabiashara waambiwe ili waweze kuyatumia ipasavyo,” alisema.

Hili lifanyike wakati ambao urasimu kwenye taasisi zote za biashara Tanzania Bara na Zanzibar ziondoe urasimu ili kuweza kusaidia wafanyabiashara kufikia malengo yao.

Pia alisisitiza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora ambazo zinaendana na mahitaji makubwa ambazo zimenunuliwa zaidi katika maonyesho hayo.

“Tunahitaji kutanua soko la bidhaa zetu na kufika mahitaji. Tunahitaji samaki kwenda nje hata ndani ya nchi pia hata dagaa hatujatosheleza, mwani nimeona mahitaji unatumika kutengeneza sabuni na dawa hivyo ni vyema kuzalisha bidhaa zenye ubora watu waridhike ili ziweze kushindana sokoni,” alisema Majaliwa.

Akizungumzia suala hilo, Fatma Hussein Abdullah ambaye ni mmoja wa waonyeshaji kutoka Zanzibar alitaka uchambuzi wa kina wa masoko kufanyika ili wajue nguvu wanaweka wapi katika uzalishaji wa bidhaa.

“Kama ni mwani tuambiwe pia mwani aina gani, mkavu, mbichi, wa unga ili twende sawa na soko husika, isijekuwa tunaleta mwani waunga kumbe unatakiwa mbichi au uliokaushwa pekee,” anasema Fatma.

Maneno yake yaliungwa mkono na Jamilla Mashaka ambaye alitaka taarifa hizo kutolewa kwa vikundi vyao vya ujasiriamali ili iwe rahisi kwao kuzipata na kuzitumia ipasavyo.