Mgogoro wa DRC, Rwanda waibua mapya wachambuzi wahoji nafasi ya EAC

Dar es Salaam. Wakati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda zikitia saini mkataba wa amani nchini Marekani ili kumaliza mzozo wa muda mrefu kati yao, wataalamu wa diplomasia wamemulika jambo hilo wakisema ni aibu na linakiuka makubaliano ya Umoja wa Afrika (AU).

Julai 27, 2025 mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili za Afrika walikutana katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mjini Washington, D.C, na kutia saini makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani na Qatar.

Mkataba huo unazitaka Serikali za DRC na Rwanda kuzindua mfumo wa ujumuishaji wa kiuchumi wa kikanda ndani ya siku 90, pamoja na kuunda mfumo wa pamoja wa uratibu wa usalama ndani ya siku 30.

Kulingana na masharti ya mkataba huo, maelfu ya wanajeshi wa Rwanda wanapaswa kuondoka DRC ndani ya miezi mitatu.

Mkataba huo unatoa matumaini ya kumaliza mapigano yaliyoongezeka kufuatia kusonga mbele kwa waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda katika mikoa yenye utajiri wa madini ya Kivu Kaskazini na Kusini.

Mgogoro huo umesababisha vifo vya maelfu na kuwalazimisha mamia ya maelfu kukimbia makazi yao tangu Januari 2025.

Mapigano hayo ni sehemu ya mzunguko wa miongo kadhaa wa mivutano na ghasia, uliochochewa na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.

“Huu ni wakati uliosubiriwa kwa muda mrefu. Hauwezi kufuta maumivu, lakini unaweza kuanza kurejesha kile ambacho migogoro imewapokonya wanawake, wanaume na watoto wengi  usalama, heshima, na matumaini ya maisha ya baadaye,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba Wagner.

“Kwa hiyo sasa kazi yetu halisi inaanza,” aliongeza wakati wa kusaini mkataba, akisisitiza kuwa makubaliano hayo yanapaswa kufuatiwa na kujiondoa kwa majeshi, haki, kurejea kwa familia zilizotawanywa, na kurejea kwa wakimbizi  kwa DRC na Rwanda.”

“Wale walioteseka zaidi wanatazama. Wanatarajia mkataba huu kuheshimiwa na hatuwezi kuwaangusha,” aliongeza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe alisema makubaliano hayo ni muhimu na ya kihistoria.

Ingawa Rwanda inakanusha madai kuwa inaunga mkono M23, Kigali imesisitiza kuwa kundi lingine la wapiganaji lililoko DRC Jeshi la Kidemokrasia la Ukombozi wa Rwanda (FDLR) linapaswa kumalizwa. FDLR lilianzishwa na Wahutu wanaohusishwa na mauaji ya Watutsi mwaka 1994.

Wakati wa kusaini mkataba, Nduhungirehe alisisitiza kuwa lazima kuwe na mwisho usioweza kurejewa na unaoweza kuthibitishwa wa DRC kuunga mkono FDLR. Mkataba unataka kundi hilo kulazimishwa kutokuwepo tena.

Akiripoti kutoka Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, mwandishi wa Al Jazeera, Alain Uaykani alisema mkataba huo ni hatua kubwa, lakini kuna mkanganyiko kuhusu kutokuwepo kwa maelezo ya lini waasi wa M23 wataondoka.

“Rwanda daima inasema si wao wanaopaswa kuwaambia M23 waondoke, kwa sababu hili ni tatizo la Congo,” alisema, akiongeza kuwa waasi hao wanateua magavana na kudhibiti viwanja vya ndege katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini, miji mikuu ya mikoa hiyo waliyoiteka Januari na Februari, mwaka huu.

Serikali ya Kinshasa, Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi wanasema Rwanda inaunga mkono M23 kwa kutuma wanajeshi na silaha.

Mkataba haujaeleza wazi mafanikio ya M23 lakini unataka Rwanda kusitisha hatua za kujilinda ilizochukua. Rwanda imetuma angalau maelfu ya wanajeshi kuvuka mpaka kuunga mkono M23, kwa mujibu wa wataalamu wa UN, wachambuzi na wanadiplomasia.

Wakati serikali za Kinshasa na Kigali zilitiliana saini makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Serikali ya DRC na waasi wa AFC/M23 jijini Doha, Qatar. Makubaliano hayo yanalenga kusitishwa kwa mapigano katika eneo la mashariki ya DRC.

Siku mbili tu baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, mapigano mapya yameripotiwa kuzuka tena katika eneo la Kivu Kusini, hali inayozua maswali kuhusu uimara na uhalisia wa makubaliano hayo mapya.

Kwa mujibu wa mashuhuda walioko katika maeneo ya Uvira na Rurambo, milio ya risasi na mizinga imekuwa ikisikika kwa nyakati tofauti tangu usiku wa kuamkia Jumapili, hali iliyowalazimu mamia ya wakazi kuyahama makazi yao na kutafuta hifadhi maeneo ya milimani karibu na mipaka ya Burundi.

“Hatukutegemea kama mapigano yangerudi haraka namna hii. Tulidhani baada ya Doha, hatimaye tungeweza kulala kwa amani,” amesema Aline Mbusa, mama wa watoto watatu, mkazi wa Rurambo aliyekimbilia eneo la Lemera.

Makubaliano ya Doha yalilenga kufungua njia ya mazungumzo ya kina, usitishaji wa uhasama, na kuandaa mazingira ya kuwarejesha wakimbizi waliokimbia machafuko ya miezi ya nyuma.

Hata hivyo, hali ilivyo sasa inaashiria changamoto kubwa katika utekelezaji wake, hasa kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi madhubuti wa kimataifa katika maeneo ya mapigano.

Wachambuzi wa usalama wa kikanda wameonya kuwa endapo hali hii haitadhibitiwa mapema, inaweza kusababisha kuvunjika kabisa kwa matumaini ya amani na kuibua wimbi jipya la wakimbizi katika eneo la maziwa makuu.

Hadi sasa, hakuna tamko rasmi kutoka kwa serikali ya DRC wala uongozi wa AFC/M23 kuhusu sababu za kuvunjika kwa hali ya utulivu, huku juhudi za upatanishi zikiendelea kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU).

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Denis Konga amesema kitendo cha DRC na Rwanda kusuluhishwa na Marekani pamoja na Qatar ni jambo la aibu na linakiuka makubaliano ya Umoja wa Afrika.

Amesema makubaliano ya AU yanaelekeza kwamba matatizo ya Afrika yatatatuliwa na Waafrika wenyewe kwa suluhisho la Kiafrika, hivyo mataifa hayo kukiuka mkataba huo wa Afrika.

“Unaporuhusu wengine kutatua matatizo yenu maana yake; kwanza, hamuheshimu yale makubaliano ya kwetu sisi wenyewe, ya Umoja wa Afrika na pia jumuiya za kikanda hususan Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),” amesema.

Amesema EAC na SADC zimekuwa zikijitahidi kutatua mgogoro huo lakini hazikuheshimiwa, jambo ambalo amesema ni baya kwani linaonyesha mataifa hayo hayaheshimu watu wa ndani, badala yake wanawaheshimu na kuwasikiliza wa nje.

Konga ameongeza kwamba Waafrika wengi wanaheshimu makubaliano yatakayoingiwa na Mataifa makubwa kama Marekani, China au Ufaransa, jambo linaloonyesha hawako thabiti katika masuala yao.

“Masilahi makubwa ya Congo yako kwa haya mataifa makubwa, ukiiangalia Qatar, inashika turufu ya Marekani, anafanya biashara na Rwanda kupitia Rwanda Airways, wana hisa nyingi. Pia, Marekani ina masilahi makubwa Congo, hasa kwenye madini mkakati,” amesema.

Mhadhiri mwingine kutoka chuoni hapo, Profesa Wetengere Kitojo amesema mkataba wa amani uliosainiwa baina ya mataifa hayo, utakuwa na manufaa makubwa kwa DRC kwa sababu mapigano yamekuwa yakirudisha nyuma shughuli za kiuchumi za wananchi.

“Kukiwa na mapigano, watu hawazalishi, uchumi wa mtu mmoja mmoja unadidimia, matokeo yake na uchumi wa taifa nao unashuka. Kwa hiyo, hii ni hatua nzuri, kinachotakiwa sasa ni utekelezaji wake ili mapigano yasiendelee,” amesema.

Kuhusu mzozo huo kutatuliwa na mataifa ya magharibi, Profesa Kitojo amesema kuna hali ya kutoaminiana ndani ya EAC, hivyo wameamua kutatua mzozo wao kwa msuluhishi ambaye wote wanamwamini na wanadhani watatendewa haki.

“Kutoaminiana ndani ya jumuiya ni changamoto nyingine inayofanya jambo hili likashughulikiwe na mataifa mengine ya mbali. Tunatakiwa kurekebisha suala hili ili kuipa heshima jumuiya katika kufanya kazi yake ya msingi,” amesema mwanazuoni huyo.