Moskow, Russia. Maofisa wa usafiri wa anga nchini Russia wameanza msako wa haraka kuipata ndege ya abiria aina ya An-24 iliyopotea kwenye rada katika eneo la Mashariki ya Mbali, karibu na mpaka wa China ikiwa na watu 50 ndani yake.
Tukio hilo limetokea asubuhi ya leo Alhamisi Julai 24, 2025 ambapo, Gavana wa Mkoa wa Amur, Vasily Orlov amesema ndege hiyo ilikuwa inakaribia kutua katika mji wa Tynda, mkoani Amur, wakati ilipopoteza mawasiliano na waongozaji.
Mkoa wa Amur upo Mashariki ya Mbali mwa Russia, ukipakana moja kwa moja na China upande wa kusini, kupitia Mto Amur ambao pia unatumika kama mpaka wa kimataifa kati ya nchi hizo mbili.
Ndege hiyo inamilikiwa na shirika la ndege la Angara, lenye makao makuu Siberia, na iliripotiwa kupotea kwenye rada muda mfupi kabla ya kutua katika mji huo uliopo karibu na mpaka wa China.
“Kwa mujibu wa taarifa za awali, kulikuwa na abiria 43, wakiwemo watoto watano na wafanyakazi wa ndege sita,” amesema Gavana Orlov.
Hata hivyo, Wizara ya Dharura ya mkoa huo imetoa idadi tofauti, ikikadiria kuwa watu waliokuwamo ndani ya ndege hiyo ni takriban watu 40.
Tukio hilo limezua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo na familia za abiria waliokuwemo, huku mamlaka zikiendelea na operesheni ya kuisaka ndege hiyo katika maeneo ya msitu na milima yenye hali ngumu ya kijiografia.
Maofisa wa usalama wa anga wamesema bado haijafahamika chanzo cha kupotea kwa ndege hiyo, huku sababu kama hali ya hewa, hitilafu ya kiufundi au makosa ya kibinadamu zikitajwa kuwa miongoni mwa zinazochunguzwa.
Endelea kufuatilia Mwananchi na mitandao yetu