Panga kuendelea Mashujaa FC, yaacha watano

UONGOZI wa maafande wa Mashujaa FC, umetangaza kuachana na nyota watano wa kikosi hicho baada ya kutofikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya, huku ikielezwa huenda ikaachana na wimbi kubwa la wachezaji ili kufanya maboresho kikosini.

Nyota waliotangazwa kuachwa na timu hiyo ni beki wa kulia, Omary Kindamba na viungo, Zubery Dabi na Ally Nassoro Iddi ‘Ufudu’, huku washambuliaji wakiwa ni Abrahaman Mussa na Mohamed Mussa aliyekuwa akiichezea kwa mkopo akitokea Simba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Abdul Tika, alisema wanaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha kikosi hicho ili kilete ushindani msimu ujao, huku wakianza pia ma-zungumzo ya kuongezea mikataba nyota wote waliomaliza.

“Wakati tunapambana kuboresha kikosi chetu kwa kuongezea nguvu wapya, pia tunaendelea ku-waongezea mikataba wengine ambao wamemaliza, taratibu hizo zimeanza na hadi kufikia Agosti 1, 2025, nafikiri tutajua kitakachotokea,” alisema Meja Tika.

Hata hivyo, Mwanaspoti limedokezewa mbali na wachezaji hao walioachwa ila wengine wanaoweza kuondoka ni beki wa kati, Ibrahim Ame aliyemaliza mkataba na kikosi hicho, ambaye inadaiwa yupo mbioni kujiunga na Mbeya City iliyopanda Ligi Kuu.

Tayari timu hiyo imefanya maboresho ya nafasi hizo, ambazo Mwanaspoti linatambua limemrejesha aliyekuwa beki wa kati wa kikosi hicho, Samson Madeleke kutoka Pamba Jiji na kiungo mkabaji, Sam-wel Onditi kutokea Kagera Sugar iliyoshuka daraja.

Wengine waliosajiliwa ni aliyekuwa winga wa KenGold, Selemani Bwenzi na mshambuliaji, Salum Kihimbwa kutokea Fountain Gate huku kiungo mshambuliaji, Omary Abdallah Omary aliyekichezea kikosi hicho akirejea tena kwa mkopo akitokea Simba.